Papa akutana na maaskofu wa Tanzania huko Vatican

 Askofu Nyaisonga ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amewaongoza maaskofu wenzake katika mazungumzo ya faragha na Papa juzi, makao makuu ya kanisa hilo jijini Vatican.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima akizungumza na gazeti hili kwa simu akiwa Vatican, alisema maaskofu hao wapo Italia katika ziara ya kichungaji inayofanyika kila baada ya miaka mitano.

“Kila baada ya miaka mitano maaskofu wote huenda hija kwenye makao makuu ya Kanisa Katoliki na kuungana na Baba Mtakatifu kwa sala na kwa mahitaji ya familia ya Mungu duniani,” alisema Padri Kitima.

“Mara ya mwisho maaskofu walikwenda Vatican 2014. Walipaswa kwenda 2019 lakini Covid-19 (Uviko) ilizuia ziara hiyo.”

Aidha, Dk Kitima alisema vilevile ujumbe huo wa maaskofu ulitembelea ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Mbali na maaskofu na Padri Kitima, wengine walioshiriki ziara hiyo iliyoanza Mei 14 mwaka huu na kumalizika leo, ni mapadri kadhaa, akiwamo Padri Chesco Msaga, Naibu Katibu Mkuu (TEC) na Padri Thomas Kiangio, msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Tanga.

Vilevile, Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF) nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo ameambatana na viongozi hao wa kidini akiwakilisha Walei Katoliki Tanzania katika Baraza la Maaskofu.

Jana, katika uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia ziara hiyo ya maaskofu wakati akianza hotuba yake na kuwashukuru viongozi mbalimbali waliofika, huku maaskofu Katoliki wakimtakia heri.

Rais Samia alisema: “…Waliniaga kwa barua wanakwenda Roma, lakini walitoa ruhusa (shughuli ya uzinduzi wa Ikulu kuendelea) na mimi nikawapa baraka zote”.


No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies