Liturujia ya Ekaristi ni sehemu ya pekee zaidi ya Misa.
Inafuata daima liturujia ya Neno na kuikamilisha kwa kumleta Yesu Kristo kati ya waamini wake kama chakula na kinywaji cha uzima kwa roho zao ili wapate nguvu na furaha kwa ajili ya kumfuata kwa kutekeleza Neno la Mungu lililotangazwa kwanza.
Mahali pake maalumu panaitwa altare (kutoka Kilatini) au madhabahu (kutoka Kiarabu), kwa sababu ukumbusho ulioachwa na Yesu katika karamu ya mwisho ni ukumbusho wa sadaka yake ya msalabani.
Liturujia ya Neno ndiyo sehemu kuu ya kwanza ya Misa, lakini inaweza kufanyika hata nje ya Misa kwa sababu kwa Wakristo Neno la Mungu ni lishe ya kwanza ya maisha ya Kiroho.
Mahali
Katika makanisa kwa kawaida kuna mahali maalumu kwa ajili ya ibada hiyo, yaani mimbari, ambayo kwa sababu hiyo inaitwa pia "meza ya Neno".
Mbali nayo, altare inaitwa "meza ya Ekaristi" kwa kuwa ndipo mkate na divai vinapoombewa vishukiwe na Roho Mtakatifu ili viwe Mwili na Damu ya Kristo, ambavyo ndivyo chakula na kinywaji cha Wakristo.
Utaratibu
Katika Kanisa Katoliki ni kawaida kusoma kwanza kutoka Agano la Kale, halafu kutoka Nyaraka za Mitume na hatimaye kutoka Injili mojawapo. Utaratibu huo unafuata ule wa utunzi wa maandiko hayo, ambapo ya mwisho ndiyo muhimu kuliko yaliyotangulia, kama katika historia ya wokovu ambapo Yesu ndiye aliyeleta divai bora mwishoni (Yoh 2:1-10).
Katikati kuna nyimbo, hasa Zaburi, ambazo zinaendana na masomo ya siku ili kuyaelewa, kuyatafakari, kuyaitikia na kuyashangilia.
Mara nyingi inafuata hotuba, halafu ungamo la imani na maombezi kwa ajili ya watu wote.
No comments
Post a Comment