NOVENA YA EKARISTI TAKATIFU

  NOVENA YA EKARISTI TAKATIFU(Mwili na Damu) 

Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele katika sadaka ya Bwana: “huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo Yesu!





(NJOO KWANGU) INAPATIKANA KTK KITABU CHA “KRISTO NI YOTE” .

 JINSI YA KUFANYA NOVENA HII: 

1.Njoo mbele ya Yesu na umwabudu.(Mbele ya Tabenaklo) 

2. Soma Maneno ya Yesu .

 3.Soma Maandiko Matakatifu ya tafakari na ujiulize mwenyewe 

 Ni sehemu ipi yenye maana kwangu?

  Ninajisikiaje ninaposoma? 

 Nitamwambia nini Yesu aliyezungumza nami binafsi kwa njia ya neno? 

4. Tumia kiitikio cha sala iliyowekwa. 

5.Sali rozari ya Huruma ya Mungu ukitolea nia fulani hasa zile Yesu analeta akilini mwako. 

. Tumia tafakari ya nyongeza na sala za nyongeza kadili utakavyopenda 

 SALA YA MWANZO:

 Sali sala ya kutubu, kisha Sali sala ya uje Roho Mtakatifu……. 

SALA YA MWISHO:Tunakimbilia ulinzi wako… 

SIKU YA KWANZA 

YESU ANAONGEA

 Njoo kwangu, najua jina lako. Wakati ule ulipokuwa unaumbwa katika tumbo la mama yako, nilikuwepo.Nilikuona hata kabla ya kuzaliwa kwako.Daima nilikuwa ninakupenda.Njoo kwangu, wewe ambaye umeelemewa nitakuburudisha, nitakupatia pumziko. Kaa na mimi na usikilize. Hii ni nyumba yangu na wewe unakaribishwa.Ninakuhitaji sana , nina hamu ya kuona unavyotambua mapendo yangu. Mapendo yangu ni kama moto unaoteketeza chuki zote, kiburi, mdhambi, n.k. Ninatamani kuyajaza maisha yako amani yangu na furaha yangu; hapa sasa niko mbele yako, mfungwa katika nyumba yangu mwenyewe. Nichukue niende na wewe katika moyo wako. Nipeleke katika nyumba yako, katika shule yako, katika ofisi yako, mtaani kwako, sauti yako, moyo wako, upeleke mapendo yangu kwa ulimwengu uliojeruhiwa. Nakusihi unipeleke katika moyo wako. 

TAFAKARI:

 Isa:61:1-4 Bwana kwa nini umekuja? Maandiko yananiambia nini kuhusu wewe? Nisomapo neno lako ninaweza kuona jinsi unavyowagusa watu na kuwaponya.Uliwalisha makundi, uliwafungua kutoka kwenye vifungo.Ulibadilisha maisha yao.Neno moja, kugusa kwa mkono wako, kuangalia kwako tu kulitosha kumrudishia mwanadamu uzima.Sasa hivi uko wapi? Mguso wako uko wapi, kuangalia kwako ambako kulirudishia uzima miili iliyovinjika, kuponya mahusiano yaliyoharibika, ulivyowatia nguvu walio dhaifu? Ninahitaji kuona! 

NIONYESHE BWANA WANGU. YESU ANAONGEA: 

Mwanangu, hili ni jibu.Niko hapa katika Ekaristia, kwa nanma ya pekee, Hapa kuna mikono ile ile ambayo ilimgusa mtu aliyekuwa amekufa na kumpa uzima, iliyogusa maji ya Baraka na kuyageuza kwa divai bora, iliyogusa macho ya kipofu. Ni mimi hapa nikiwa na uwezo ule ule wa kuponya kila ugonjwa wa mwanadamu, kulituliza tufani katika maisha yako .Mara nyingine tena siku ya leo ninataka unipeleke nyumbani, nienda na mimi kufanya kazi, nitakuwa pamoja nawe, nitakubariki, ndipo nawe utakuwa Baraka kwa wengine!Je tutakwenda pamoja?

 SALA: Yesu njoo na utembee pamoja nami. Ninakutolea moyo wangu uwe kama altare, ninakukaribisha Bwana. Ni mapendo yaliyotakiwa kutaka kuishi ndani mwangu na kumtumia! Kwa muda mrefu nimeyabeba matatizo na maumivu na magonjwa lakini sikujua mbele yako katika Sakramenti Tukufu ambako umekuwa ukiningojea. Ninakushukuru kwamba sasa nimetambua mapendo yako na uwezo wako katika Ekaristi. Ndiyo, Bwana, nitakupeleka kwa wengine. Njoo uishi ndani mwangu Bwana na unitumie mimi kugusa maisha ya wengine .Amina (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA PILI 

KRISTO ANAONGEA 

Karibu mwanangu.Nilijua utakuja. Ninayo mengi ya kukupatia. Ninazo zawadi nyingi zilizo katika hazina kwa ajili yako na wale uwapendao.Ninao uwezo, mapendo ya kufanya kila ndoto ifanikiwe . Ndoto ambazo zinaleta mapendo na amani na uponyaji kwa dunia iliyokata tamaa. Kwa nini mwanangu watu mamilioni waende bila uponyaji na kufariki katika maumivu yasiyotakwa? Wakati mikono hii ambayo iligusa mwili wa mkoma na akatakasika, iko hapa tu kimya au bila kutumika. Ni lini watu wangu watakuja kwangu na kukaa tu mbele yangu. Huko kuna chuki nyingi katika ulimwengu kuna kutotendeana haki kwingi, mateso mengi na kuna uwezo mmoja, mtu mmoja anayeweza kukuponya na kurudishia ulimwengu kila alichoiba shetani.Uwezo huo uko hapa. 

 TAFAKARI

 Nguvu ya Mungu daima inapatikana.Kwa kuja na kuwa mbele ya Ekaristi ninachota nguvu hizo.Nguvu za Mungu zinapatikana kwa ajili yetu katika kila tukio la maisha yetu. Mungu alimwambia Yoshua, “Siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha”(Yos 1:5).Paulo aliandika: “sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote”(2The 3:16). (Rudia aya hizi za Maandiko Matakatifu na ufanye yazame zaidi ndani mwako, kumbuka kila ahadi kwa ajili ya hitaji lako maalumu) 

YESU ANAONGEA 

Niko hapa mwanangu.Mkono wangu umekuelekea ili kukusaidia ushinde. Nguvu zangu zinakutosha. Niangalie mimi katika Ekaristi. Niko hapa nikiwa naishi kati yenu kuponya yale ya zamani na kuyakomboa yake yajayo.Ninakuita kwa jina lako.Je unanipenda?NDIYO? 

Hapo uyapokee mapendo yangu, amani yangu.Chukua mapendo yangu, amani yangu, pamoja nawe. Ubaki kimya katika uwepo wangu. 

SALA Bwana Yesu ujio wako ulibadilisha mkondo wa historia.Ninajua kuwa wewe ni mwanga ambao kamwe hautafifia. Hakutakuwa na giza wala huzuni itakayoweza kuzima mng”aro huo. Yesu mapendo yako yatashinda, mapendo hayo yatashinda chuki, uchungu na magomvi.Kuta ndefu haiwezi kukuzuia wewe Bwana, silaha za vita haziwezi kuzuia kuenea kwa amani yako.Hapa kuna uwezo, nguvu ambazo zinaweza kuleta uponyaji na amani katika maisha yetu, nguvu ambazo zitatuweka huru dhidi ya kila kinyume. Bwana, ninakuomba amani Lakini ninatambua kuwa katika upofu wangu ninakatalia wengine paji la amani ambalo mimi ninalitafuta kutoka kwako. Nitegemeeje kuona mkono wako wa kuume wa ushindi unaonishikilia mimi (Isa41:10) wakati nimefunga moyo wangu na mikono yangu dhidi ya ndugu yangu? Bwana nimekuwa kiziwi kwa mwaliko wako wa toba.Nimekuwa kipofu kwa matendo yangu ya binafsi .Unihurumie mimi Bwana nimekukosea wewe unifundishe niwe mtu ambaye unapenda niwe.Amina (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA TATU

YESU ANAONGEA

 Njoo kwangu, weka mkono wako katika mkono wangu. Usiwe na woga .Wewe ni wa pekee kwangu.Ninalijua jina lako; ninataka kuona uso wako. Ninataka kukufuta machozi yako, wewe ni wangu wa pekee. Vile tangu nilipokuumba hapa duniani, hajawahi kuwepo mwingine kama wewe, wala hatakuwepo mwingine kama wewe. Nyanyua kichwa chako anagalia juu, nipe sifa kwa ajili ya zawadi ya maisha yako. Nipe sifa kwa sababu wewe uliumbwa wa pekee. Kwa nini unakuwa na wasiwasi?Kwa nini unajisikia upweke?Nini kinachokusababisha upoteze amani? Nieleze kinachokusibu na hata ukafanya moyo wako ubaki mtupu, nawe utakuwa na amani yangu. Je, kumbukumbu za zamani zinakuumiza? Je kuna dhambi ya siri inayotafuna moyo wako na kukusumbua? Njoo, nipatie mimi.Kwa wema nitakusamehe kosa lako la zamani. 

TAFAKARI: 

Lk 4:40-41 Fikiria watu wale unaowajua ambao wamekwama katika kukata tamaaa kujihurumia, na mfadhaiko, walete kwa Yesu, namna hiyo utakuwa chombo chake cha uponyaji.Je, unamjua mtu yeyote ambaye anabebana na chuki katika moyo wake au pengine mawazo ya kulipiza kisasi?Au wale walevi wa madawa ya kulevya, walevi wa pombe, mashoga? Wote walete kwa Yesu. Alikuja kuwaletea uhuru. Bado yu hai hapa kwenye altare. Hebu, tumchukulie katika maisha ya wanafamilia wetu na katika ulimwengu wote. Majeraha yanapona kwa Bwana aliyeteseka kwa ajili yetu. “Huwaponya waliopondeka moyo, na kuziganga jeraha zao” (Zab 147:3) na hunipatia pumziko, “Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza”(Zab 23:2). “Nami nitawaokoa katika mahali pote waliotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitatafuta waliopotea, Nitawarudisha waliofukuzwa, Nitawafunga waliovunjika , Nitawatia nguvu wagonjwa” (Eze 34:12,16). (Zingatia ile aya amabayo inakufariji zaidi na mruhusu Yesu akufariji) 

SALA: 

Ee Yesu, njoo utembee pamoja nasi kila asubuhi; jua linawaka na matumaini yanang”ara: nasi tuchukue matumaini hayo kwa watu wengine. Bwana, siku ya leo uniongoze kwa watu wale unaotaka kuongea nao, kunipitia. Ninajua kuwa hata ninavyoruhusu unitumie mimi, uwepo wako maishani mwangu utakuwa dhahiri zaidi. Nitakavyozidi kuwatuliza watu wengine, ndivyo nitakavyozidi kupata faraja yako na uponyi. Bwana bado niko na woga. Pengine nitasita, pengine hatua zangu zitakuwa dhaifu, pengine bidii yangu itafifia, Bwana, uwe karibu nami. Nishikilie Yesu, hasa nitakapolegea kukushika. Usiruhusu siku zinazopita, miezi na miaka zinikute nimekusahau. Fanya kila siku inayopita inikute nikiwa chini ya miguu yako nikichota nguvu, faraja na kitulizo kutoka kwako. Bwana, uwabariki watu wote walio na woga kukutana na wewe. Na hao pia wakujue wewe kama ulivyojionyesha kwangu. Ndiyo Bwana, nao pia wakujue kuwa mkombozi wao, mponyaji wao na amani yao isiyo na mwisho.Amina (Ruhusu amani ya Yesu ipite, kaa mbele yake ukivuta pumzi, pumua amani Yake) (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA NNE 

KRISTO ANAONGEA

 Makaribisho mara mia moja! Moyo wangu una hamu kubwa ya kukuona weweunaingia. Sahau unyeneyekevu wa kujidai na wa uongo amabao unakufanya usistahili kuingia ndani. Ninatambua kushindwa kwako. Hakuna kilicho cha siri kwangu mwanangu; licha ya udhaifu wako wote, bado ninakutaka. Ninakupatia mapendo yangu, msamaha wangu, kukubali kwangu, hata unaponitolea toba yako. Ni roho yangu ambayo ilielekeza hatua zako hapa kwangu. Nimekuteua uwe tarishi wangu kwa ulimwengu. Kumbuka nilivyomchagua Maria Magdalena kuwaambia wengine kuwa nimefufuka, sasa ninakuchagua kuuambia ulimwengu kwamba niko hai na ninasubiri hapa katika Ekaristi kwa ajili yao. Niko hapa kabisa, kwa mapendo katika Moyo wangu, uwezo katika mikono yangu kwa ajili ya kubadilisha maisha, kuponya hali ya kukata tama, kusamehe dhambi, kuwalisha wenye njaa, kuwaletea amani wale wanaosumbuka. Mwanangu, inaumizaje moyo wangu kuona mwanangu akiteseka naye akikataa kuja hapa ili kuondolewa maumivu katika mwili, akili na roho. Tafadhali nenda na wape wengine habari hii njema, washirikishe vile unavyojisikia, na nyakati hizi zina maana gani kwako.Nakuomba uwe tarishi wa mapendo, nitakuwa pamoja na wewe. 

TAFAKARI: 

Kristo katika Ekaristi huzama ndani kabisa ya maisha ya wale wanaokaa mbele yake na kuusikia upole wake na mapendo ya kudumu yasiyosahaulika. Anatugusa kiasi ambacho si rahisi kuelewa akibadilisha maisha kimuujiza. Bila kujali ni dini gani mtu anayoishika, wala hali ya mtu zamani ilikuwaje.Mapendo yake yanakumbatia wote. Nguvu ikaayo katika ukimya wa altare inatoka na kubariki ulimwengu. Mungu huona katika mioyo yetu na kutuwezesha na kutuweka sawa. “Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mt 6:21). “Mwanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana hutazama moyo” (1Sam 16:7). Nami nitawapa moyo mmoja, name nitatia roho mpya ndani yao; name nitauondoa moyo wa kijiwe katika mili yao, name nitawapa moyo wa nyama, ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, name nitakuwa Mungu wao (Eze 11:19-20). Sitapungukiwa kabisa, wala sitakuacha kabisa (Ebr 13:5b) S

ALA Yesu pendwa sana,ninakushukuru kwa kunipatia siku hii ya leo, uhakika wako wa msamaha wako wa upendo na wa kutukubaloi. Inapendezaje kujua wema wa mapendo Yako.Licha ya udhaifu wangu, kuanguka kwangu bado tu unanipenda. Bwana ninasikia ukiniita ili nitoke nje na kushirikisha mapendo yako nyumbani, kwa wale ninaokutna nao. Bwana, ninatambua watu wengi wanaoishi katika giza, upweke, na wanavumilia mateso kwa sababu hawajawahi kusikia kwamba wewe ni Mponyaji. Bwana nimeshindwa kuachia uwezo wako kwa watu wengine. Leo nimejua kwa mara nyingi nitakapoachia nguvu yako kwa wenginendivyo nitakavyopokea Baraka zako na kijitolea mwenyewe kama chombo chako cha kupeleka Baraka kwa watu wengine. Watafute watuwengine amabo wanatafuta mapendo na ukweli. Waongoze kwenye mwanga wako. Watafute waabuduo miungu ya uongo. Unawapenda na ulikufa kwa ajili yao. Jalia kwamba kwa njiaya sala zetu watabarikiwa na kuletwa karibu na wewe, watafute wale wanaoteseka kimwili, kiroho na kiakili, na wafariji katika majaribu yao. Bwana uwe mwenye huruma kwa wale waliogandamiza na kuumiza watu wengine. Wapeni moyo mpya, na fanya mwanga wako uangaze maneno yangu yote na matendo. Amina (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA TANO 

 KRISTO ANAONGEA 

Njoo kwangu usiogope. Kitu cha pekee ninachotaka kuwaambia siku ya leo; Je unajua kuwa unaponitembelea utakuja kupewa tuzo? Hyupo anayekuja kwnagu akaondoka mikono mitupu. Utaweza kusikia habari njema; moyo wako utajazwa kwa mapendo na furaha. Utaona kuwa akili yako itapata mwanga. Utakapokaa kwa utulivu mbele yangu, utatatajirishwa zaidi ya unavyofikiria. Ninapenda uelewe hivi: Wewe ni mtu wa maana na wa pekee kwangu. Ninalijua jina lako. Jina lako limechorwa kwenye kiganja cha mkono wangu. Usijali vile unavyofikiria, ninakuona wewe kuwa mpendwa mmoja Yule niliyemwaga Damu kwa ajili yake na nikafa. Nimekubariki wewe kwa namna ya pekee. Nimekupa mapaji na uyatumiapo mapaji haya,yatazidi kuongezeka. Unakumbuka kijana aliyenipa mikate 5 na samaki 2. Namna hiyo niliwalisha watu wangapi? Nitakupokea chochote utakachonipa mimi na nitakitumia. Nipatie mikono yako, uinyooshe unielekezee, ili niweze kuibariki na kuifanya daima iwe wazi kwa ajili ya kushirikiana. Nipatie macho yako, ili niweze kuyabariki yaweze kuona na kutambua mahitaji yaw engine. Nipatie sauti yako, nitaibariki na kuitumia ili wale watakaokusikia, wajazwe furaha na mapendo. Nipe moyo wako name huo nikikupatia wa kwangu, ili niweze kupenda kupitia.

 TAFAKARI 

Toa nawe utapewa katika kipimo mara mbili, hatuwezi kumzidi Mungu katika ukarimu.Jinsi nikaavyo katika ukimya na kumtolea sehemu aitumie kama apendavyo, Moyo wake wa Kiekaristi unafurahia na kwa kukurudishia, ana ahidi Baraka kuzidi ufahamu wetu. Nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu (Isa41:10). Atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu (Flp 4:19). Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu (Flp 4:13). Sitapungukiwa kabisa, wala sitakuacha kabisa (Ebr 13:5b). Chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu (Rum 8:39). Mimi Bwana wako niko pamoja na wewe popote uendako. SALA Bwana ni vipi nimekuwa kipofu namna hii? Nimetesekaje kila wakati hata kukata tama kwa sababu siji kwako.Nyakati zingine, maisha yangu yamekuwa na mtitririko wa siku za kutokuwa na furaha zikikusikia ukiniita. Bwana, ninatakiwa kuwa mkweli kwako. Kulikuwa na nyakati ambapo nilijisikia umeniacha nawe kwamba sikuwa mwema ya kutosha na kwamba hujali kunisika tena. Unihurumie Ee Yesu. Siku ya leo ninaona jinsi nilivyokuwa mjinga, wewe ni mpole sana na rafiki mpendevu ambaye nina heri kuwa nawe. Wewe unayohamu moja ya kutoa, na kutoa, na badala yake unanitaka nitoe kidogo na hata kidogo hicho, ninashindwa kukupa. Bwana, ninakupa moyo wangu. Njoo Bwana, dondosha chini kuta za wivu, hasira , ubaridi, kujipendelea, sema neon la uponyaji katika moyo wangu, legeza maumivu ya ndani, na tuliza maumivu niliyonayo. Bwana, kwa niaba ya ndugu zangu na dada zangu duniani kote, ninakukaribisha wewe katika nyumba zetu. Nyumba zetu zinatoa kilio kwako. Wazazi waliotengana sasa hivi wanataniana. Maneno ambayo hapo awali yalihamasisha upendo sasa linaiua. Uwe na huruma Yesu kwa familia zote zirudishie amani na mapendo. Bwana njoo tena, uongee tena, uponye tena na uguse tena. Amina (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA SITA 

KRISTO ANAONGEA: 

Karibu rafiki yangu sana nimekuwa nikikusubiri wewe. Ninayofuraha sana kwa kuwa umeamua kuja kutumia muda pamoja na mimi. Ni furaha iliyoje na faraja inayoletwa ndani ya mwangu Mtakatifu. Kukufanya wewe ujiandae na kuacha kila kitu na kutumia nyakati hizi pamoja na mimi. Kusema kweli nitakutuza kwa kiwango amabacho huwezi kikitegemea. Moyo wangu unatoka kuwaelekea wanangu wanaoteseka. Ninyi ni watu mnaoteseka. Niko hapa wanangu ili kuwafariji kutokana na majonzi. Msiogope, elekeza mateso yenu na majonzi kwangu. Niruhusuni niwapende kwa mapendo ambayo hayana mwisho na yaliyo safi. Ni mapendo peke yake ambayo yanaweza kuwaridhisha katika mahitaji yenu yote. Kuweni na amani wapendwa wangu sitashindwa kuwatimizia mahitaji yenu yote. Kuweni wenye amani wapendwa wangu kamwe sitawatelekeza. Wakati mwingine utafikiri sijibuharaka sala zako, pengine kama hakuna kinachotokea. Laiti wanangu kama mngelikuwa na matumaini katika mimi! Niamini. Ninawapendeni kabisa bila masharti yoyote. Kuweni na imani name, yaamini mapendo yangu, kuweni na imani na uwezo wangu. Siwezi kuwaelekezi vya kutosha kuhusu MAPENDO yangu. Ninawapenda sana na kamwe kabisa sitawaacheni yatima. Niruhusu niyagange madonda ya roho zenu. Kubali niyafunike kwa damu yangu yenye thamani kubwa, ambayo ni mapendo yangu ninayomwaga kuwatakasa na kuwasafisha ninyi. Ninazo neema nyingi za kuwapa wanangu, lakini walio wengi wanakataa kuja kwangu kuzipokea na kuponywa. Je utakwenda uwafikishie mwaliko wangu? Niruhusu nikutumie ili kuwafikia hao.

 TAFAKARI

 Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa?Je, yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu? Kwa sababu hiyo Bwana asema hihi “ukirudi ndipo mimi nitakporejeza upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha dhambini katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa change” (Yer 15:18-19). “Bwana anafadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema” (Zab 145:8). “Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena” (Eze 37:23). “Nitawatakasa watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. “Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hakutaka” (Mt 23:37). “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa Moyo” (Hos 14:4) SALA Yesu ninakushukuru kwa kunifanya nijione kwmba ninaalikwa kwenye nyumba yako. Nimekuwa nikizurura sehemu moja kwenda nyingine, toka kwa mtu huyu kwenda kwa Yule, nikifukuzia goli moja baada ya linguine. Wakati Fulani ninapata kuridhishwa kwa wazo la raha za muda tu lakini nikiwa bado katika shida zile zile. Bado wakati mwingine najisikia mtupu moyoni na akiliinakosa mafanikio .Wakati mwingine sitambui ni kitu gani nahitaji.Kitu nilichokuwa nikiitafuta, ni Yesu, sasa nimejua. Ilinifanya niwepo kwa ajili yako tu na kila hitaji la uwepo wangu kwako ninapata kitulizo. Sasa Napata wazo la mafanikio, ya kufika nyumbani na Yesu ninakusudia nitakaa. Bwana ninatambua kuwa uko hapa, katika wewe sala zangu zote zitajibiwa. Ninakubali mbinju, muda na namna amabyo utanijibu mimi, kwani ninaridhika kuwa unanijua, unajua kilicho chemakwangu na ambacho kinaweza kunidhuru.Mapendo yako kwangu kamwe hayawezi kuwa sababu ya kunipa n’nge pale ninapokuomba samaki. Yesu ninakutumainia ninakusadiki, Ninaamini mapendo yako kwa ajili yangu, ninajikabidhi kabisa kwa mapendo yako. (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

 SIKU YA SABA 

KRISTO ANAONGEA:

 Njooni kwangu nyote mlio na furaha kwani nitafanya furaha ikamilike kikamilifu. Ninapenda kuwafundisha ni kitu gani kinachoondoa furaha ya kweli. Chuki zote, maudhi, kinyongo. Magomvi yasiyoisha, choyo, ubinafsi hizo ndizo sababu za kupora furaha. Jifunzeni kwangu, jinsi ya kutunza mioyo yenu safi, kuwa na uzuri na wema. Njooni kwangu nyie mlio na huzuni. Je? Mnafikiri maisha hayajawatendea hai? Je, mipango yako imeshindwa? Je? Wale ulioweka matumaini kwao wamekusitisha? Je, maisha yenu yanaoekana kwenda mrama? Wanangu uko kwenye nafasi sahihi sasa. Ongea nieleze, toa yote yaliyo moyoni mwako, Roho wangu anawajaza Amani, faraja na maelekezo. Kaa mbele yangu kadiri unavyotaka na utakapojisikia umefarijika na kuimarishwa, toka nje, nenda uwe mwakilishi wangu. Watafute wale waliosababisha mateso kwa wengine, wale waliopoteza matumaini. Mimi ninaitwa Mponyaji aliyejeruhiwa. Wewe uliyeteseka pia ni mponyaji unayeweza kuwaletea wengine huruma na mapendo niliyokupa. Sasa nimekuchagua wewe kuwa mtume wangu. Ulikuwa na mateso ambayo yamekuwa ni mafunzo kwako yamekufanya usikilize na kuleta uponyaji na tumaini kwa wengine. Ewe mwanangu siku nyingi nilikuwa nimejificha, kwa msaada wako, na uwezo wangu ukweli na mapendo ya ufalme wangu vinaweza kuachiwa ili kuenea. Wewe ungetakaje kuwa mtume wangu? 

 TAFAKARI 

“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda”(Yh15:16). “Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”(Isa 6:8). “kabla sijakuumba katika tumbo nilikujua na hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa”(Yer1:5). “Alimkuta katika nchi ya ukame, na katika jangwa tupu litishalo. Alimzunguka, akamtunza, akamuhifadhi kama mboni ya jicho” (Kum 32:10). “Enendeni ulimwengui mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe” (Mk16:15). 

 SALA Yesu, kuja kwako kupokea faraja na baraka ni kitu kimoja, lakini kupokea agizo ni kitu kingine kama Musa. Mimi pia nataka kutafuta kisingizio kama Isaya. Mimi natambua kuwa sistahili kama yeremia, ninajikuta bila kujitayarisha. Bado naweza kukuta macho yako yakipenya ndani kabisa ya roho yangu. Ninaweza kukusikia ukiita kutoka kwenye ubinafsi wangu na kiburi, ninajua visingizio vyangu si vya kweli. Akili yangu inaelekea Kalvari na kukuona ukiteseka kwa ajili ya wanadamu. Nitakwenda Ee Bwana. Najua ni hali ngumu lakini uliniahidi kuwa hutaniacha niwe peke yagu. Yesu njoo uguse moyo wangu ulio baridi kwa cheche ya mapendo yako. Fungua macho yetu na legeza ndimi zetu ili tutangaze habari njema ya wokovu, Amani na mapendo. Uwezo wako katika ekaristi hauna mipaka. Kwa uwezo huo tutaweza kutoka. Utabariki siku ya leo na ujaze mioyo yetu kwa mapendo yako mengi na yaliyo safi. Bwana achia nguvu zako za kuponya zitoke kwenye altare hii. (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

SIKU YA NANE 

KRISTO ANAONGEA

Ewe mdogo njoo nikaribie – kaa karibu na mimi na shusha pumzi kwenye mapendo yangu makubwa na yasiyo na masharti. Kwa ajili yako nikawa mwanadamu Kwa ajili yako nikaishi Kwa ajili yako nikafa Kwa ajili yako nikafufuka. Kwa ajili yako ninaishi katika Altare. Ninajua maumivu ya siri kwa kila kumbukumbu, hofu isiyoonekana iliyofichika ndani ya moyo wako, mashaka, wasiwasi, kukata tamaa katika kilamoyo viko mbele yangu. Ninajua njaa ya wenye njaa, machozi ya wapweke, upofu wa waliokataliwa na uchungu wa waliofungwa. Nimefanya kila teso la mwanadamu na hitaji lake liwe langu, ikiwa nguvu na upendo wangu utajulikana!njoo tafadhali njoo, usiombe yanayokuhusu mwenyewe tu, lakini pia kwa ajili ya watu wengine. Niletee wenye njaa, walemavu, walioanguka, wanaogandamizwa, wanaoshambuliwa, wenye kiburi,niletee watu wote. Nimekuja kuwaletea wongofu na wokovu. Niamini mimi, wanangu, kuweni mitume wangu katika sala na matendo. 

 TAFAKARI: 

“Nami nikatafuta tu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi nisije ikaharibu, lakini sikuona mtu”(Eze 22:30). “Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana na usiku. Ninyi wenye kumkubusha Bwana msiwe kimya” (Isa 62:6). “Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza” (Ayu 42:10). SALA Bwana sifa na shukrani ni zako kwa ajili ya mambo yote uliyoyafanya mbele yetu. Siwezi kuona shaka juu ya mapendo yako hasa ninapokuona hapa altareni. Inua kiwango cha ufahamu wagu Ee Bwana, ili niweze kuleta kwa njia ya sala, mahitaji ya ulimwengu. Bwana wewe liyewalisha makundi, uwe na huruma kwa wenye njaa na wale walio katika hali ya dhiki ya kiuchumi, watimizie mahitaji yao kulingana na utajiri wako wa huruma. Unakuja kuleta Amani na mapendo na bado yote yaliyonizunguka ninaona mateso na vurugu, umwangaji wad au na majanga. Nani awezaye kutuokoa kutokana na wingi wa mateso na kukata tamaa? Ni wewe pekee. Wewe pekee uliyemwondosha shetani na kumponda. Ulifufuka kutoka kaburini na kushinda kifo. Hapa kwenye altare nguvu yako haimaliziki. Mapendo yako ni yenye nguvu na hayana mwisho. Utuponyeshe na utusamehe, utuweke huru, nayo nuvu ya mapendo yako itulize hasira. Ponya uchungu wote, nyamazisha silaha zote za vita, waondolee mbali mashetani wote wa fujo na mateso waweke watu wako huru Ee Bwana. Amina. (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) 

 SIKU TA TISA 

YESU ANAONGEA

 Furahini wanangu wadogo na toeni shukrani na sifa. Muda uliokaa pamoja na mimi haukuwa bure. Ni heri iliyoje kwako kuwa na uzima. Baraka kuu uliyopokea na paji la imani itakufanya ukamilike. Tayari umeshatambua kupata fadhili, maombi mengine yaliyofanyika yatasikiwa na kujibiwa kwa wakati. Jibu sala, ponya majeraha, lakini Zaidi ninaomba uniruhusu nifanye mambo kwa namna yangu – uniruhusu nijibu sala nionavyo – kwa wakati wangu. Kuweni na Imani na mimi, ninaelewa hali nzima, ninaweza kuona mbele siwezi kuruhusu maumivu yasiyo ya lazima. Njoo kwangu mara nyingi unavyoweza wakati ukiwa na kazi nyingi, walau ingia ndani kwa kunitembelea. Daima nitakukaribisha, nitakufundisha, nitakukumbatia na kukuweka huru, nitakujaza roho wangu na utaweza kurudi tena kwenye mazingira yako ukiwa mtulivu na mwenye Amani, ukiweza kukabiliana a matatizo ya siku husika. Nitakuwa pamoja na wewe ili kutuliza upepo mkali katika maisha yako. Katika siku chache hizi za mwisho umeweza kuona uwezo wangu. Shuhudia kwa mapedo yangu na nguvu. Waeleze watu wengine kuhusu mapendo yangu kwa ajili yao katika Ekaristi na muhimu zaidi waweze kuja kuniona mimi Mungu mpole, mpendelevu na wakati huo Mungu mwenye uwezo, katika maisha yenu. Eneza mwaliko wangu kwa watu wengine na rudi tena maana ninayo mambo mengi niliyowawekea.

 TARAKARI

 “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu mjifunze kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na nyenyekevu wa moyo nanyi mtapata raha nafsini mwenu”(Mt 11:28-29). “basi nyeyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yako”(1Pet 5:6-7). “Bwana akubarikie na kukulinda , Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake na kukupa Amani”(Hes 6:2426). “Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa. Usiongope wala usifadhaike kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako”( Yos 1:9) SALA: Bwana, umegusa moyo wangu katika siku hizi 9 nilipokuwa na wewe. Ni vyema kweli kuwa katika nyumba ya Bwana!Bwana, ninakusifu kutokana na Amani na Baraka nyingi nilizipokea (Zitaje Baraka ulizopokea). Maneno uliyonipatia ni roho na ni mwanga wa maisha. Kusema kweli Bwana nimenyanyuliwa na kuhuishwa. Nilikuja kwako nikiwa mdhambi, nilikuja kwako wakati akili yangu ilikuwa imepondeka kwa wasiwasi. Wakati roho yangu imejaa maumivu kutokana na upweke, majeraha, wakati moyo wangu unahuzunika kwa ajili ya wale nipendao. Nilikuja wakati mwingine mwili wangu ukiwa na uchovu na maumivu. Yesu wangu, ulinipokea. Ulinipa makao katika moyo wako wa Kiekaristia –Ulinipenda na kuniponya na kunimwagia Roho wako kama maji ya maua. Na sasa Bwana mpendwa sana pamoja na moyo wa shukrani, ninainama mbele yako nikisema Asante sana. (Sali Rozari ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya nia zako) YESU ANAONGEA Mwanangu, si lazima ujue mambo mengi ndipo unifurahishe; wewe unipende sana tu. Ongea na mimi kama ungekuwa unaongea na mama yako aliyekushika mikononi mwake. Je, huna mtu wa kumpedekeza kwangu? Taja majina ya jamaa zako, ya rafiki zako (baada ya kila jina eleza kile unachotaka nimtendee). Niombe mambo mengi, mimi napenda mioyo yenye ukarimu ambayo wao hujisahau kwa ajili ya watu wengine. Nieleze kuhusu wale walio maskini ambao unapenda niwasaidie, wagonjwa ambao umewaona wakiteseka, wadhambi ambao ungetamani wapate wongofu, watu waliofarakana na wewe ambao wewe unataka kurudisha uhusiano, kwa ajili ya hao wote, Sali sala ya dhati. Nikumbushe kuwa nilishatoa ahadi ya kujibu kila sala inayokuja kwangu kutoka moyoni na hakika sala ya dhati ambayo tunasali kwa ajili ya wale tunaowapenda, na wanaotupenda. Je, huna fadhli unazotaka kuomba kwa ajili yako mwenyewe? Andika, endapo unataka orodha ndefu ya matamanio yako mahitaji yote ya roho yako – njoo na uisome mbele yangu. Niambie kiasi unavyojihurumia, ulivyo na kiburi, mkorofi, kiasi ulivyo mbinafsi, jinsi ulivyo mwoga, jinsi ulivyo mzembe, niombe mimi nikusaidie kujirekebisha. Ewe mwanangu maskini! Usiwe na haya! Mbinguni kuna watakatifu wengi waliokuwa na makosa hayo kama wewe; waliniomba , na polepole wakaweza kupona. Usisite kuniomba kumbukumbu nzuri ya mafanikio. Ninaweza kuwapeni kila kitu na daima pale paji hilo litakapoweza kumfanya mtu awe mtakatifu Zaidi. Je, siku ya leo unataka nini mwanangu? Lo! Ungelielewa kiasi gani ninatamani kukufanya uwe mtu mwema! Mimi nasoma ndani kabisa ya moyo wako. Wanadamu hudanganyika, lakini si Mungu, kuweni wazi. Je, unao uamuzi wa kuepuka nafasi za dhambi, kuachana na kitu kinachokufaya upotoke kutosoma vitabu ambavyo vinasisimua mawazo yako; kuachana na urafiki wako na mtu yule ambaye si mshika dini, ambaye ukaribu naye unafadhaisha Amani ya roho yako? Utaenda na kuwa mkarimu kwa yule mwenzako ambaye alikuudhi? Vizuri mwanangu, nenda sasa endelea na kazi yako ya kila siku, uwe kimya, mwenye huruma, mvumilivu, mkarimu na hapo kasha uniletee moyo ulio na uchaji Zaidi na wenye upendo. Kesho nitakuwa na fadhili mpya kwa ajili yako. WIMBO WA KUMTUKUZA MUNGU. Atukuzwe Mungu; Litukuzwe Jina lake Takatifu; Atukuzwe Yesu Kristo, Mungu kweli na mtu kweli Litukuzwe Jina la Yesu; Utukuzwe Moyo wake Mtakatifu; Itukuzwe Damu yake Takatifu; Atukuzwe Yesu katika Sakrament Takatifu ya Altre; Atukuzwe Roho Mtakatifu Mfarriji; Atukuzwe Mama wa Mungu, Maria Mtakatifu; Atukuzwe Maria aliyekingiwa dhambi ya asili; Atukuzwe maria aliyepalizwa Mbinguni; Litukuzwe jina la Maria, Bikira na Mama; Atukuzwe Mtakatifu Yosefu, mhumba wake mwenye usafi kamili; Atukuzwe Mungu katika Malaika wake na watakatifu wake. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies