ROZARI NI NINI NA HISTORIA FUPI YA ROZARI



“Rozari ni sala nzuri sana na yenye utajiri wa neema, ni sala inayogusa kwa karibu Moyo Safi wa Mama wa Mungu na ikiwa unataka amani itawale katika nyumba zenu, salini Rozari katika familia” 

Utangulizi

Kila mwezi Oktoba (10) waamini Wakatoliki wanaalikwa kusali Rozari kwa mwezi mzima. Lengo kubwa ni kumweshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria kwa maombezi yake ya kimama kwetu wanadamu. Mwezi wa 10 ni fursa nyingine tena ya kumwendea Mama Bikira Maria na kumshirikisha furaha, shukrani, taabu, changamoto na matarajio yetu kwa njia ya Rozari Takatifu ambayo hutupa nafasi ya kutafakari mafumbo ya maisha ya Yesu na Maria katika safari ya wokovu wetu. Hivyo tukiwa kwenye Mwezi wa Rozari nimeona ni vyema nikuletee walau kwa ufupi historia ya Rozari Takatifu.

 Asili ya neno “Rozari”

Neno la Kiingereza “rosary” linatokana na neno la Kilatini “Rozarium” lenye maana ya “bustani ya mawaridi” (rose garden) au “taji ya mawaridi”. Kwa kadiri ya desturi ya watu wa Ulaya kupeana maua ya mawaridi ni moja ya matendo yenye lengo la kuonesha upendo wa hali ya juu kwa mtu Fulani, hasa wakati wa furaha au huzuni; mawaridi pia ni zawadi kubwa ya upendo hasa baina ya wapenzi. Sisi Wakristo Mama Bikira Maria ni mpenzi wetu na zawadi kubwa tunayoweza kumpa ni “kusali rozari” ambayo ndiyo “mawaridi yetu kwake”. Kwa kadiri ya mapokeo mawaridi, hasa meupe yanamwakilisha Bikira Maria asiye na doa, yaani ni mweupe kama waridi jeupe.

 Kwa nini mwezi wa 10 ni mwezi wa Rozari?

Kanisa limeweka mwezi Mei na Oktoba kuwa miezi ya kumweshimu Mama Bikira Maria. Wengi wetu hufahamu tu mwezi Oktoba. Mwezi Mei ni mwezi wa Bikira Maria kwa kuwa Bikira Maria aliwatokea Lucia, Francisco na Jacinta huko Fatima Ureno kwa mara ya kwanza Mei 13, 1917 ujumbe mkuu ukiwa kuhangaikia wokovu wa roho za binadamu kwa njia ya kusali rozari na ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria.

Mwezi wa 10 ni mwezi wa kusali Rozari Takatifu. Kuchanguliwa kwa mwezi wa 10 kuna msingi wake katika historia ya Kanisa. Waislam wa Kituruki miaka ya 1500 waliamua kutumia mwanya wa vuguvugu la kujitenga kwa Waprotestanti kutoka Kanisa Katoliki. Hivyo waliamua kuvamia nchi za Ulaya ili kueneza dini yao kwa nguvu ya upanga na vita kwa kuwalazimisha Wakristo kuwa Waislam. Oktoba 7, 1571 Waislam wa Kituruki waliamua kuivamia Italy kwa kuanzisha vita ya baharini iliyojulikana kama Vita vya Lepanto (Ugiriki). Baba Mtakatifu wa wakati huo alikuwa Pius V. Baba Mtakatifu alijua wazi kuwa Waislam walikuwa ni wengi kwa idadi kuliko Wakristo na ya kuwa Waislam walikuwa na meli nyingi za kivita kuliko Wakristo. Hata hivyo Baba Mtakatifu aliamuru jeshi lake likisaidiwa na wanajeshi kutoka Spain kwenda baharini kupambana na Waislam. Baba Mtakatifu aliamuru kila askari abebe Rozari na kuisali wanapokuwa vitani majini; pia aliamuru wananchi wa Italia waliobaki majumbani wafanye maandamo makubwa huku wakisali Rozari kuomba msaada wa Bikira Maria ili Wakristo washinde vita. Yeye mwenyewe alisali Rozari siku hiyo ya Oktoba 7. Muda si mrefu habari zilimfikia Baba Mtakatifu kuwa Wakristo wameshinda vita na kati ya meli 242 za Waislam zimesalia meli 12 tu huku jumla ya Waislam 30,000 wakiwa wameuwa, takribani 8,000 wamejeruhiwa au kutekwa. Kwa upande wa Wakristo ni watu 7,500 tu waliokuwa ama wameuawa au wamejeruhiwa au kutekwa ambao baadaye wengi wao walifanikiwa kutoroka. Baba Mtakatifu Pius V alitamka kuwa ushindi huo haujatokana na weledi wa askari wala ubora wa vifaa vya kivita bali ni ushindi uliotokana na maombezi ya Bikira Maria wa Rozari. Kutokana na ushindi huo dhidi ya Waislam Baba Mtakatifu Pius V alianzisha rasmi Sherehe ya Mama Yetu wa Ushindi mwaka 1572. Mwaka 1573 Baba Mtakatifu Gregory XIII aliibadilisha jina sherehe hiyo na kuipa jina la Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu. Mwaka 1884 Baba Mtakatifu Leo XIII alitangaza rasmi kuwa mwezi wote wa kumi utakuwa mwezi wa kusali Rozari Takatifu akiwa na kumbukumbu ya ushindi ambao Wakristo waliupata dhidi ya Waislam katika vita vya Lepanto tarehe 7 Oktoba 1571. Lengo kubwa la kutangaza mwezi wa 10 kuwa mwezi wa Rozari lilikuwa kumweshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria ambaye kwa maombezi yake Wakristo walipata ushindi Oktoba 7, 1571.

Kwa nini Bikira Maria anajishughulisha na wokovu wa wanadamu?

Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho na kufanywa Malkia huko mbinguni. Kwa nini asikae huko akatulia na kuendelea kufurahia kumwona Mungu uso kwa uso? Kwa nini anawatokea watu duniani? Jibu ni rahisi sana: Kwanza, Bikira Maria, kwa kumuona Mungu kama alivyo, anafahamu furaha isiyo na kifani ya kumwona Mungu na anataka kila mtu apate furaha hiyo; na ndiyo maana hawezi kutulia mbinguni kwa kuwa anatamani kila mmoja aionje furaha hiyo hasa wakosefu. Ndiyo maana anapowatokea watu duniani anatoa ujumbe kwa watu kufanya toba, kusali rozari, kupokea mateso kama njia ya kupata wokovu, kuombea marehemu wa toharani na kuonya wakosefu kubadili matendo yao. Pili, Bikira Maria anajishughulisha na wokovu wa wanadamu kwa kuwa alikabidhiwa jukumu hilo na mwanaye Yesu Kristo “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao” (Yoh. 19:26). Sisi sote tunawakilishwa na Yohane; sisi sote ni wana wa Maria. Hivyo Yesu hapa anamaanisha “Mama! Tazama, watoto wako”. Neno “Tazama” lina maana kubwa sana: kututunza, kutushughulikia na kutuangalia kwa namna ya pekee. Hivyo Bikira Maria anaendelea siku zote kututunza, kutushughulikia na kutuangalia kwa namna ya pekee kwa maombezi yake ya kimama, kwa kutuelekeza nini tufanye pindi anapotokea kwa baadhi ya watu.

 “Tazama, huyu ndiye mama yako” (Yoh. 19:27)

Yesu anamwambia Yohane amtazame mama yake (Bikira Maria). Yohane anatuwakilisha sisi sote. Sisi sote tumekabidhiwa kwa Bikira Maria kama Mama yetu. Je, tumtazameje Bikira Maria? Tutamtazama Bikira Maria kwa kumpenda, kumheshimu na zaidi ya yote kwa kusali Rozari Takatifu ambayo kiini chake ni tafakari ya mafumbo juu ya maisha ya Yesu na Bikira Maria. Kwa nini tusali Rozari? Je, Rozari ina faida gani?

• Rozari inatuwezesha kuwa na ufahamu kamili kuhusu Yesu siku kwa siku

• Rozari inatakasa roho zetu

• Rozari inatupatia ushindi dhidi ya adui zetu

• Rozari inatuwezesha kuishi maisha ya fadhila

• Rozari inawasha ndani yetu moyo wa mapendo kwa Bwana Wetu Yesu Kristo

• Rozari inatutajirisha kwa neema na mastahili

• Rozari inatuwezesha kupata yale tunayohitaji kutoka kwa Mungu

• Rozari inawezesha kufunguliwa kwa roho zilizopo toharani.

• Rozari inatutia nguvu tuwapo katika madhaifu na changamoto za kimwili na kiroho.

 Matokeo ya Kusali Rozari

Kwa hakika Rozari ni sala yenye nguvu sana. Ukijiwekea mazoea ya kuisali utaona uzuri wa Rozari na kamwe hutaiacha. Zamani niliona kusali Rozari ni mzigo, ni kupoteza muda na kama kero tupu. Lakini kila siku nazidi kuonja uzuri na nguvu ya Sala ya Rozari. Muda mzuri wa kusali Rozari ya binafsi, kwa kadiri ya uzoefu wangu binafsi, ni alfajiri kwani akili huwa imetulia sana. Hata hivyo, kila mtu anaweza kutenga muda wake atakaoona unafaa kwake. Kwa njia ya kusali Rozari:

• Wadhambi wanasamehewa

• Roho zenye kiu zinaburudishwa

• Magumu yanafanywa kuwa mepesi

• Wanaopitia majaribu wanapata amani

• Maskini wanapata msaada

• Wenye mahangaiko wanapata faraja

• Roho za marehemu toharani zinapunguziwa mateso na zingine kufunguliwa

Ee Mama Mpendelevu sana, utujalie nguvu ya kuweza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya

wokovu wetu na wa dunia nzima, Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies