ROZARI YA MIKAELI MALAIKA MKUU

ROZARI YA MALAIKA MKUU MIKAELI

Rozari ya Malaika Mkuu Mikaeli ni sala nzuri sana ya kumheshimu huyu Malaika Mkuu pamoja na makundi yote tisa ya Malaika. Kuendana na jinsi tunavyofunuliwa katika Maandiko Matakatifu, makundi haya tofauti tofauti ya Malaika hujipanga kuanzia karibu sana na Kiti cha Enzi alipo Mwenyezi Mungu, kwenda chini tulipo sisi wanadamu. Makundi hayo kuanzia juu kwenda chini ni Maserafi, Makerubi, Wenye Enzi, Watawala, Wenye Nguvu, Wenye Mamlaka, Wakuu, Malaika Wakuu na Malaika.

Asili ya Rozari hii ni maono aliyopata Mtumishi wa Mungu Antonia d’Astonac, ambaye alitokewa na Malaika Mkuu Mikaeli aliyemfundisha sala za Rozari hii kwa kumwelekeza kuwa anataka aheshimiwe kwa salamu tisa kufuatana na makundi tisa ya Malaika.

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu aliahidi kuwa yeyote anayefanya ibada hii kwa heshima, akaribiapo Meza Takatifu, atasindikizwa na Malaika tisa, mmoja kutoka kila kundi la Malaika. Zaidi ya hayo, kwa kusali rozari hii, aliahidi msaada wa daima, na kwamba Malaika watamsaidia mwenye kuisali duniani na kumtoa toharani akifariki, yeye pamoja na jamaa zake.Ee Mungu unielekezee msaada, Ee Bwana unisaidie hima!

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.

Sali Baba Yetu (mara nne) kwa heshima ya Malaika Wakuu, Mtakatifu Mikaeli, Mtakatifu Gabriel, Mtakatifu Rafaeli na Malaika Mlinzi.

1. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Mikaeli;

Baba Yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina

2. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Gabrieli; Baba Yetu, …..
3. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Rafaeli; Baba Yetu, …..
4. Kwa heshima ya Malaika Wangu Mlinzi; Baba Yetu, ……

Sali Baba Yetu moja na Salamu Maria tatu baada ya kila salamu katika tisa zifuatazo kwa heshima ya Makundi Tisa ya Malaika

Baba Yetu (mara moja, – tazama hapo juu)

Salamu Maria
Salamu Maria umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

1. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya kundi la Serafin, Bwana awashe mioyoni mwetu moto wa mapendo kamili. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

2. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Kerubin, Bwana atuwezeshe kuacha njia mbaya na kuenenda katika njia ya ukamilifu wa kiKristo. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

3. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Enzi, Bwana atujalie roho ya unyofu na unyenyekevu wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

4. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Watawala, Bwana atujalie neema ya kushinda maasi yetu na tamaa mbaya. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

5. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Nguvu, Bwana atukinge na vishawishi na mitego ya shetani. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

6. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Mamlaka, Bwana atukinge na mwovu wala tusianguke vishawishini. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

7. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wakuu, Bwana atujalie kuwa na roho ya utii wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

8. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika Wakuu, Bwana atudumishe katika imani na katika kazi zote njema ili tujaliwe utukufu wa Milele. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

9. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika, Bwana atujalie ulinzi wao duniani hapa na baadaye watuongoze kwenye furaha za Mbinguni. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies