MASOMO YA MISA JULAI 29, 2023; JUMAMOSI: JUMA LA 16 LA MWAKA


 

JULAI 29, 2023; JUMAMOSI: JUMA LA 16 LA MWAKA

Mt. Marta
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Kut 24:3-8
Musa aliwaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili za Israeli, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili akapeleka vijana na wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe.
Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15

  1. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
    Toka maawio ya jua hata machweo yake.
    Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
    Mungu amemulika.
    (K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
  2. Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
    Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
    Na mbingu zitatangaza haki yake,
    Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)
  3. Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;
    Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
    Ukaniite siku ya mateso;
    Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

INJILI: Mt 13:24-30
Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La, msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

TAFAKARI:
UPENDO KWA MUNGU NA KWA JIRANI: Katika somo la kwanza leo tunaalikwa kuishi fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani. Upendo ni fadhila ya Kimungu inayotuwezesha kumpenda Mungu na kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe. Imani yetu kwa Mungu inawezeshwa na kukamilishwa kwa njia ya upendo tulio nao kwa wenzetu. Ili kuonyesha kweli tunampenda Mungu, sharti tuwapende kwanza wenzetu tunaoishi nao. Katika Injili tunakumbushwa kuwa imani inayoongozwa na kutawaliwa na upendo itatupeleka katika ufufuko ambao utatuwezesha kuishi na Bwana milele. Yesu ni kielelezo cha maisha ya upendo kwani kwa upendo wake kwetu alikuwa tayari kufa kifo cha aibu msalabani ili kutukomboa. Zaidi ya hayo aliwapenda watu wote bila ubaguzi kwani pamoja na kwamba yeye ni Mungu alijishughulisha kabisa na watu wa kawaida katika jamii. Ndiyo maana alifika kuwafariji wafiwa. Upendo wa kweli unatutaka kuvaa hali za wenzetu katika jamii.

SALA: Ee Mungu naomba uwashe ndani mwangu fadhila ya mapendo. Amina.

( Hide )

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies