Sakramenti ya ndoa ni nini?



SAKRAMENTI YA NDOA

Sakramenti ya ndoa ndio yenye kuwaunganisha wakristo wawili mume namke waliopendana kwa hiari bila shuruti au vitisho au kizuizi kwa kuwapa neema ya kuishi pamoja kitakatifu wakiwalea watoto wao katika utakatifu

Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya nani?
Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya Yesu na Kanisa lake.
“Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi arusi, mke wa Mwanakondoo” (Ufu 21:9).
Wakiwa na ndoa halisi, mume na mke waliobatizwa ni ishara wazi ya hao wanaarusi wawili wasioonekana.
“Kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Ef 5:24-25).
Ndiyo sababu Mkatoliki hawezi kufunga ndoa bila ya kuhusisha Kanisa na kufuata taratibu zake.

Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu gani?
Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu ya umuhimu wa familia kwa ustawi wa mume na mke, watoto, jamii na ufalme wa Mungu, na kwa sababu ya uzito wa majukumu yanayohusika.
“Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwepo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake” (Yoh 2:1-2), akaleta divai bora ya ndoa sakramenti badala ya ndoa ya kimaumbile.
Hivyo ametuandalia neema tuweze kushinda “ugumu wa mioyo” (Math 19:8) unaohatarisha daima uzuri wa mpango wa Mungu kuhusu upendo mwaminifu katika ndoa. “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwa 1:31).

Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa nini?

Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa;
1. Uhuru wa kila mmoja
2. Matangazo ya ndoa
3. Wachumba wawe na nia ya kweli ya kuoana
4. Mafundisho na semina ya ndoa
5. Wasiwe na kizuizi chochote cha ndoa
6. Wasikae suria na wapokee Sakramenti ya Kitubio

Vizuizi vya ndoa ni vipi?

Vizuizi vya ndoa ni;
1. Upungufu wa umri
2. Uhanithi
3. Ndoa awali halali
4. Tofauti za dini au upagani
5. Daraja Takatifu
6. Nadhiri
7. Utekaji au kutumia nguvu
8. Taksiri au Jinai au Mauaji ya mwenzi wa ndoa
9. Uhusiano wa damu
10. Uhusiano wa ndoa
11. Ugoni au uhawara
12. Kuasili mtoto au Uhusiano wa kisheria

Mtu aweza kupokea Sakramenti ya ndoa zaidi ya mara moja?

Ndiyo, mwenzi akifa yule aliyebaki yupo huru kufunga ndoa tena (1Kor 7:39)

Ndoa mchanganyiko maana yake ni nini?

Ndoa mchanganyiko ni ndoa kati ya Mkristo Mkatoliki na Mkristo asiye Mkatoliki

Je, ndoa halali inaweza kuvunjwa?

Hapana, Hakuna yeyote anayeweza kuvunja ndoa halali isipokuwa kifo. (Mt 19:4-6)

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies