IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?

 

IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?

Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni “NINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABA” inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hilo ni kweli kwa sababu jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika “Ibada ya Kuabudu Msalaba” – jina ambalo nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!

NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA KUU?
Wanachofanya Wakatoliki Siku ya Ijumaa Kuu ni KUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani? WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: “HUU NDIO MTI WA MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.” Waamini wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu WOKOVU – YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia “YESHUA”, maana yake “WOKOVU” (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta wokovu, anafanya makosa makubwa!

Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani, wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi, Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko kwenye majumba yao na makanisani.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies