JE WAKRISTU WAKATOLIKI WANAABUDU SANAMU


Kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya wakatoliki kwamba wanaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani?
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, “Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Sheria hiyo inapatikana pia katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: “Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Ni kutokana na vifungu hivyo vya Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.

KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI KUABUDIWA?
Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote; ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri kwamba ndiye aliyetuumba na “ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tuko!” (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu, kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.

MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA YA SANAMU
Ili kufahamu vema kinachofanywa na Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema. Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, 

NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).

KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU AU PICHA?

Wakatolikihawaabudu sanamu kwa sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo, hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia (Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu – “Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!” (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. “Mungu wetu yuko mbinguni, hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. … Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu” (Zab.115:3-9). Pia kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi (Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao (1Pet.4:3-4).

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies