KUKAZA MACHO YETU KWA KRISTO NA UTUKUFU WAKE!

 Tafakari ya kila siku

Jumapili Agosti 6, 2023
Juma la 18 la Mwaka

Sikukuu ya Kung’ara Bwana wetu

Dan 7:9-10, 13-14; 
Zab 96:1-2, 5-6, 9; 
2 Pet 1:16-19;
Lk 9: 28-36



KUKAZA MACHO YETU KWA KRISTO NA UTUKUFU WAKE!

Kuna nyakati mbili katika Kalenda ya Lirtujia tunapopata nafasi ya kutafakari juu ya tukio la Kung’ara Bwana, jumapili ya pili ya kwaresima kudhihirisha Umungu wa Kristo kabla ya mateso na kifo, na siku nyingine ni tarehe kama ya leo, tunaadhimisha kutukuka kwa utukufu wa Kristo. Zaidi ya yote Kung’ara Bwana kunaonesha ukweli wa Utatu Mtakatifu: Baba katika sauti, Mwana katika Yesu, Roho katika wingu jeupe linalo nga’ara. Mungu hapa anatupa nafasi yakuona ukuu wake katika maisha ya Utatu. Mt. Leo Mkuu anasema “Lengo kuu la Kung’ara Bwana ilikuwa ni kuondoa ndani ya mioyo ya wafuasi aibu ya Msalaba”. Kati ya mambo mengi tuangalie mambo mawili leo; la kwanza, Yesu ni Mungu kamili na mwanadamu kamili. Maisha yake na mafundisho yake hayajaletwa na mwanadamu. Maneno yake sio tuu maneno ya kawaida. Ni Mungu mwenyewe anayeongea na sisi kupitia Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo. La pili, tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na tunaitwa katika maisha ya furaha ya milele, mwili na roho mbinguni. Siku hizi katika jamii zetu tunaona wengi hawajali utu wa mwanadamu (utoaji mimba, kuua mtu kwa kumchoma sindano za dawa kwakisingizio kwamba anateseka mno bora apumzike-najiuliza unawezaje kuondoa mateso ya mtu kwa kumuua?, tunaona pia sheria za kuwanyonga watu, vita na mengine mengi). Tutambue na tusisahau kwamba mwanadamu ni kiumbe pekee duniani ambacho Mungu amependa mwenyewe kwa kumuita kushiriki, kwa njia ya akili, utashi na upendo katika maisha ya Kimungu.

Ilikuwa ni kipindi cha baridi kali asubuhi kijana mmoja anayeitwa Filipo alikuwa akigawa daftari ndogo katika kijiji cha jirani. Na jalada la daftari hizi ndogo liliandikwa “Mungu anakupenda, kuwa na Imani kwake”. Alikuwa ametembelea nyumba zote isipokuwa moja tu. Alienda katika nyumba hiyo akagonga kengele cha mlango. Lakini hakukuwa na jibu. Lakini mara ya tatu alivyo gonga tena kengele dada mmoja akatokea. Kijana huyu mdogo anayeitwa Filipo akaonesha tabasamu kubwa akamwambia “Mama, Mungu anakupenda, kuwa na Imani naye”. Yule dada akacheka na kufunga mlango. Miaka michache baadae yule dada akatoa ushuhuda katika vyombo vya habari akasema ‘leo nipo hai kwasababu ya yule kijana aliyekuja kwangu na kuniambia kwamba Mungu ananipenda niwe na Imani naye”. Nilimuona Yesu akiongea na mimi kupitia kijana huyu. Nilikuwa na uchungu ndani mwangu na kukata tamaa kubwa. Nilitaka kujinyonga lakini kijana huyu aliniokoa. Ingawaje sijui yupo wapi leo, lakini napenda kumshukuru kwa kunikumbusha kwamba Mungu ananipenda mimi. Mimi ni wa thamani kubwa katika mikono yake.

Kuna hali nyingi sana katika maisha yetu zinazo tufanya sisi tukose furaha na nyakati nyingine tuwe na furaha. Hali hizi zinamfanya mtu kukata tamaa na kutaka hata kujinyonga na kujimaliza. Watu wengi wadogo na wazee hushindwa kupata maana ya maisha yao, jambo la mwisho ambalo wanapenda kulifanya nikukomesha maisha yao tu. Lakini liturjia ya leo inatuita ili tuweze kuwa na matumaini kwa Yesu katika hali za ugumu wetu.

Katika somo la kwanza , nabii Danieli anaona ndoto. Anaona utawala wa ufalme wa Mungu. Ilikuwa ni kipindi ambacho Wayahudi walikuwa wakiteseka kipindi cha Mfalme Antikus wa IV. Ili kuwapa Wayahudi matumaini katika mateso yao, wanaambiwa kwamba utawala wa Mungu utatawala milele.

Somo la pili la Mtume Petro, ujumbe huu ulilengwa kwa Kanisa la Roma, ambalo walikuwa katika mashaka na madhulumu huku wakisubiri ujio wa pili wa Bwana. Petro anawaambia watu waliopoteza matumaini na kutikiswa katika Imani yao, anawaambia kwamba utawala wa Mungu upo kati yao na kwamba Bwana atakuja.Wanapaswa kuwa na uvumilivu kama mlinzi anavyo ngojea mapambazuko na jua kuchomoza.

katika somo la Injili tunasikia juu ya Yesu kungara sura. Kabla ya Yesu kungara sura alipanda mlimani kusali na kuongea na Baba yake. Ingawaje Yesu alitambua kwamba atateseka na kufa msalabani alienda Mlimani kusali kwa Baba yake wa Mbinguni, “ninafanya mapenzi yako” tofauti kubwa kati yetu na Yesu ni kwamba Yesu yeye daima alimuuliza Baba yake “Baba unapenda mimi nifanye nini” lakini sisi tunauliza kila siku “mimi ninataka kufanya nini?”

Wakati Yesu alivyoenda mlimani walitokea, Musa na Elia. Nabii Musa alichukuliwa kuwa mtu mkubwa kati ya watu walioleta sheria katika Agano la Kale. Alikuwa mtu wa pekee aliyeleta sheria ya Mungu kati ya watu wake Israeli. Elia alikuwa mkuu kati ya manabii wote kwa njia yake, sauti ya Mungu iliongea na watu kwa njia ya pekee. Kwa njia ya kutokea kwa hawa manabii wawili mitume walitambua kwamba Yesu alikuwa Masiha wa kweli ambaye amekuja kuwakomboa watu wote kutoka katika mateso na matatizo.

Kutokea kwa wingu jeupe, kunajibu maswali yote aliyoomba Yesu kutoka kwa Baba yake. Ilikuwa ni ishara kwamba Baba yupo naye katika utume wake katika kutangaza ufalme wa Mungu na katika magumu yake. Ni tukio hili katika kungara uso linamfanya Kristo aweze kutembea katika njia ya Mateso. Mungu pia anaongea nasi kwa njia ya neno wake. Je, tupo makini namna ghani katika kusikiliza sauti hii?

Ujumbe wa kungara uso kwa Bwana unatupatia ujumbe wa matumaini na nguvu. Wakati wa wasi wasi na mashaka, njia ya kufika kwetu kwa Mungu, kunategemea sana kusikiliza maneno haya ya Mungu na kubadilika kwamba “huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikilizeni yeye”. Kungara uso kwa Bwana kunatusaidia pia kubadilisha mawazo yetu kutoka katika hali ya kidunia na kwenda katika hali ya Mbinguni. Furaha ya ulimwengu hudumu kwa muda tu na hivyo hutuacha katika mashaka na wasi wasi bali tukipata furaha kutoka kwa Yesu tutabaki katika furaha hiyo milele. Tunaitwa kumwamini Mungu daima. Ni katika kuishi katika neema hizi za Kristo tutakuwa na matumaini kwamba siku ya mwisho kutakuwa na neema na sio hukumu ya kuangamizwa. Kila ibaada ya Misa takatifu ni mwaliko kwetu wa kufanya maisha yetu upya. Ni wakati wakuhisi uwepo wake wakati mkate na divai vinavyo geuka na kuwa mwili na damu yake. Tunaomba mwili na damu yake tunayopokea itubadilishe na kutufanya wapya.

Tafakari leo juu ya uzuri wa Mungu wa kutaka kubadilisha mioyo yetu. Anataka ukaze macho yako katika utukufu huu wake wa daima hata katika mateso unayopitia katika maisha yako.

Sala: Bwana, Ninaomba nione utukufu wako na utukufu ambao wewe mwenyewe umeuweka katika roho yangu. Ninaomba macho yangu yakaze daima katika utukufu wa neema hii. Ninaomba nikuone wewe daima katika utukufu huu, hata katika hali ngumu. Yesu, nakuamini wewe. Amina

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies