KWA NINI KANISA KATOLIKI LINAWEKA SANAMU KANISANI

Kwa nini wakatoliki wanaweka sanamu Kanisani?
Tunaweka sanamu Kanisani kwa sababu tunaheshimu anayewakilishwa na sanamu hiyo kwa mfano Yesu Kristo, Mama Bikira Maria, Malaika na Watakatifu; na kamwe hatuziabudu. (Kutoka 25:18-22)
Hata Waisraeli kwenye hekalu lao walikua na sanamu kama tunavyosoma hapa;
“18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. (Kutoka 25 :18-22.)“

Kwa nini tunasali mbele ya Picha/Sanamu na Hasa kufanya Ishara ya msalaba?

Tunasali mbela ya sanamu kwa sababu tunaamini sanamu inaakisi uwepo wa mhusika aliyechorwa au kuchongwa kwenye hiyo sanamu/picha. Ndio maana wakatoliki wanasali kwenye picha au sanamu iliyobarikiwa tuu kwa sababu Sanamu inapobarikiwa inaombewa uwepo wayule anayewakilishwa pale.
Tunafanya ishara ya msalaba kwenye sanamu kama sala ya utangulizi ambayo inathibitisha kuwa hatuabudu kile kilichoko pale bali kile tunachokifanya tunakifanya huku tukikiri Umungu na Heshima ya Utatu Mtakatifu (Mungu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.). Vile vile tunamtukuza Mungu katika Utatu Mtakatifu kwa sababu ya yule anayewakilishwa na picha au sanamu.

Kwa hiyo kama Mungu mwenyewe aliagiza Sanamu za Malaika zichongwe na kusema atakua hapo na kuongea na watu wake. Je sio vyema zaidi kuwa na sanamu na Picha ya Mwanae wa Pekee Yesu Kristo na kuongea na Mungu mbele yake kama alitaka ya malaika ambao sio Mungu?
Mfano mwingine ni pale Mungu alivyomwabia Musa achonge Sanamu ya Nyoka wa shaba.
“BWANA akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti, ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.’’ 9Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu ye yote alipoumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.” (Hesabu 21:8-9).
Kwa Mfano huu Je tunaweza kusema kuwa sanamu ya nyoka ina nguvu ya uponyaji kuliko ya Yesu aliye Mungu? Kumbuka hapa watu walioona sanamu hii ya nyoka hawakuponywa na nguvu ya sanamu ya shaba bali kwa nguvu ya neema ya Mungu kupitia Imani kwa Mungu. Kwa hiyo unaposali mbele ya picha au sanamu hautegemei nguvu ya sanamu bali unategemea neema ya Mungu kwa njia ya Imani yako kwa Mungu.
Kama vile Sanamu hii ya nyoka aliyoagiza Mungu iwekwe ilivyowekwa kwa nia ya uponyaji kwa yule aitazamaye vivyo hivyo Sanamu na Picha za Kanisani zinawekwa kwa nia maalumu na kwa neema maalumu. Ndiyo maana hazifanani. Na zinabarikiwa kwa kuombewa Baraka Ili zizae neema kwa wanaozitumia.

Sanamu au picha sio haramu bali maana ya hiyo sanamu au picha ndio inaiharamisha.
Kuna tofauti kati ya kuabudu na kuheshimu. Wakatoliki wanaweka sanamu kwa heshima na sio kwa kuabudu, ndio maana unaposali mbele ya picha ya Yesu hausali ee sanamu nisaidie bali unasema ee Yesu nisaidie.
Je tuseme tunamwabudu Raisi kwa kuheshimu picha yake kwa kuiinamia? Je tunaabudu bendera kwa kuheshimu na kupigia saluti? Je taratibu zabunge za kutoa heshima na taratibu za mahakama ni kuabudu?. Je kuapa mbele ya picha ya Raisi ni kumuabudu Raisi? Je kuapa na Biblia ni kuabudu Biblia? Je tunapobusu Biblia na kuitunza kwa heshima tunaiabudu? Tofauti ya Biblia na sanamu ni nini? Je, kwenye Biblia kinachoheshimiwa ni karatasi au maana ya yale maneno kwenye karatasi. 

Pengine usingeheshimu kama hujajua kuyasoma.
Kuna tofauti gani kati ya biblia yenye Maandishi na msalaba wa kuchonga wenye kuonyesha kile kinachosemwa na biblia? kama unaweza kuheshimu biblia yenye karatasi tena pale unapoweza kuzisoma na pengine ungeizarau kama ni ya lugha tofauti na hujui kilichoandikwa? Je Msalaba uliobeba maana ya kile kilichoandikwa kwenye Biblia unaona si kitu? Kama Kinachoheshimiwa kwenye Biblia sio karatasi bali maana maneno yaliyoandikwa vivyo hivyo kinachoheshimiwa kwenye picha au sanamu sio chuma yake au mti ukiochongwa bali ni maana ya hiyo sanamu.
Hii ndio maana nasema kuna tofauti ya kuabudu na kuheshimu.

Kumbuka kuwa picha au sanamu yoyote ya Kikatoliki lazima ibarikiwe kwanza ndio uweze Kusali mbele yake. Inapobarikiwa inaombewa uwepo wa yule anayewakilishwa na picha/sanamu hiyo uwe pale sanamu ilipo na anayesali pale sala yake Ifike kwa mlengwa anayeonekana kwa ishara ya sanamu/picha. Kwa Mfano askofu au padri anapobariki sanamu ya Yesu anaomba kuwa “Yesu awepo pale kwenye sanamu na Neema zake”, kwa hiyo yeyote anayesali mbele ya sanamu hiyo anaamini kuwa Yesu yuko pale na anasali Mbele yake. Kwa hiyo kinachopewa heshima sio ile sanamu bali ni yule anayeonekana kwa ishara ya ile sanamu au picha.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies