KWA NINI TUNASALI

Sala ni nini?
Sala ni kuinua mioyo yetu kwa Mungu na kuongea nae. Kuongea maana yake ni kusema na Kusikiliza. Sala sio kuongea tuu, sala ni kuongea na kusikiliza. Mungu anatualika tuongee nae kwa kusema na kusikiliza. Kwenye Biblia tunasoma Hivi;
“Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua”.(Yeremia 33:3)
Vile tunavyokuwa na juhudi ya kusali kwa kusema mbele ya Mungu ndivyo hivyo hivyo tunatakiwa tuwe na juhudi ya kumsikiliza Mungu kile anachotuambia.
Tunaweza kumsikiliza Mungu ndani kabisa ya Mioyo yetu, mara nyingine kwa kupitia dhamira zetu, kupitia watu wengine na kupitia neno lake (Biblia). Tuombe neema ya kutambua sauti yake anaposema nasi ili tuweze kumsikiliza na kutengeneza mahusiano mazuri kati yetu na yeye.
Mungu ni Baba yetu, anatupenda sana na yupo tayari kutusikiliza wakati wote ndio maana Mungu anatualika kwa kutuambia;
“Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. (Isaya 1:18)
Tudumu katika sala daima kwa sababu njia ya sala ndipo tunaweza kusema yale tunayotaka mbele ya Mungu na kusikia yale anayotaka Mungu.

Kwa nini tunasali?
Tunasali ili kudumisha mahusiano yetu na Mungu na ili kutimiza wajibu wetu Mbele ya Mungu. Sababu kuu za kusali ni;Kumwabudu Mungu,
Kumshukuru Mungu,
Kuomba neema na baraka kwa ajili yetu na wenzetu,
Kuomba msamaha,
Kumsifu na kumtukuza Mungu

Ni nyakati gani zafaa kwa sala?
Nyakati zote zafaa kwa sala hasa:
1. Asubuhi na jioni
2. Kabla na baada ya kula
3. Kila Dominika
4. Sikukuu za amri
5. Kabla na baada ya kazi
6. Katika kishawishi

Ni zipi sala Muhimu kwa Mkristo?

Sala muhimu kwa Mkristo ni;
1. Misa Takatifu
2. Baraka ya Sakramenti Kuu
3. Litania Takatifu
4. Njia ya Msalaba
5. Rozari Takatifu
6.Novena

Sala zina faida gani? Kwa nini watu tunasali?

Sala zina faida hizi;
1. Zinaleta neema nyingi
2. Zinatuimarisha ili kushinda vishawishi na dhambi
3. Zinatuunganisha na Mungu
4. Zinatudumisha katika kutenda mema

Yesu ametufundisha kusali vipi?
Yesu ametufundisha kusali akitueleza misimamo ambayo tuwe nayo.
“Upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako… Waombeeni wanaowaudhi… Msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu” (Math 5:24,44; 6:5).
“Mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, ‘Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi’. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki” (Lk 18:13-14).

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies