MAFUNDISHO KUHUSU UBATIZO


Sakramenti ya ubatizo ni nini?

Sakramenti ya Ubatizo ni Sakramenti yenye kuondoa dhambi ya asili pamoja na dhambi nyingine zote tulizotenda, kufufua roho zetu kwa kututia uzima wa Mungu, Kutuandika Wakristu Watoto wateule wa Mungu na wa Kanisa.

Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
“Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27).

Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu lini?
Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, sio tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18).
Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame.
“Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).

Je, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji ulikuwa sakramenti?

Hapana, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote.
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11).
Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5)

Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni zipi?
Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake.
“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27).
Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatizwe “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19).
Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho.

Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ipi?
Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai.
Sisi ambao tulishiriki kifumbo kifo na ufufuko wake tukapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, tunaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapotulisha na kutunywesha Mwili na Damu yake ili tushiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi.
“Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57).
Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani mwetu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.

Msimamizi wa ubatizo ana wajibu gani?

Msimamizi wa ubatizo ana wajibu hizi;
1. Kutoa mfano mzuri wa maisha ya Kikristo
2. Kumuongoza mbatizwa katika maisha ya Ukristo
3. Kumuombea mbatizwa
4. Kushirikiana na wazazi katika malezi

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies