MASOMO YA MISA IJUMAAA, 1 SEPT 2023

 SOMO 1: 1The. 4:1-8

Ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama mataifa wasiomjua Mungu. Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 97:1-2, 5-6, 10-12

  1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
    Visiwa vingi na vifurahi.
    Mawingu na giza vyamzunguka,
    Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
    (K) Enyi wenye haki, mfurahini Bwana.
  2. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
    Mbele za Bwana wa dunia yote.
    Mbingu zimetangaza haki yake,
    Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
  3. Enyi mmpendao Bwana,uchukieni uovu;
    Huwalinda nafsi zao watauwa wake,
    Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki. (K)
  4. Nuru imemzukia mwenye haki,
    Na furaha wanyofu wa moyo.
    Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana,
    Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)

INJILI: Mt 25:1-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.
Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni kwa sababu hamwijui siku wala saa.

TAFAKARI:
IMANI YENU IWE HAI: Kwa mfano wa wanawali kumi, Kristo anawatahadharisha mitume kuwa tayari kwa ujio wake wa pili. Wanawali watano waliojiandaa kwa mafuta ya ziada wanafananishwa na waumini hai wanaomgoja Bwana kwa kukesha. Wanawali watano wapumbavu ni mfano wa waumini waliojiandaa kushiriki karamu ya Mbinguni lakini kadiri muda unavyokwenda, imani yao inafifia hadi kushindwa kumlaki Bwana ajapo. Mtume Paulo anawahimiza Wathesalonike kujitakatifuza daima kwa kumpendeza Mungu na kuepukana na tamaa na kuishi kwa upendo kwa ndugu ili kuwa katika utakaso. Katika ulimwengu wa sasa uliojaa shinikizo za kila namna za utandawazi, waumini wapo hatarini kufuata tamaa za miili na akili zao na kuacha imani yao kufifia. Masomo haya yatukumbushe kwamba hata katika dhoruba za mabadiliko, waumini wanatarajiwa kuilinda imani yao imara na hai, na kuepukana na kila namna ya ushawishi wa vionjo vya mwili. Mt. Monika alijitahidi sana kumwombea na kumshauri mwanawe kuepukana na anasa hadi kuwa Mt. Agostino.

SALA: Ee Bwana, Utujalie kushinda vishawishi, tudumishe imani kwako, ili ujapo tukubalike katika karamu ya Mbinguni. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies