MASOMO YA MISA JUMATATU 28,2023


 MASOMO YA MISA, JUMATATU, AGOSTI 28, 2023

JUMA LA 21 LA MWAKA 

Kumbukumbu ya Mt. Agustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

SOMO I
1The. 1:2-5, 8-10

Twamshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu.

Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na ktika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.

Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lolote. Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 149:1-6 (K) 4

(K) Bwana awaridhia watu wake.

Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao. (K)

Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao. (K)

SHANGILIO
Zab. 130: 5

Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.

INJILI
Mt. 23: 13-22

Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake: Ole wenu waandishi ns Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunuga Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au ile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies