MASOMO YA MISA, JUMATATU, AGOSTI 7, 2023






JUMATATU JUMA LA 18 LA MWAKA 

SOMO 1 
Hes. 11 :4-15

Wana wa Israeli walilia wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hi; mana tu.

Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtarna, na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamaa yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.

Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika.

Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote? je! ni mimi nilivewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto aamwaye, wende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? kwani wanililia, wakisema, Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.

Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu 


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 81 :11-16 (K) 1

(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.

Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, 
Waenende katika mashauri yao. (K)

Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Ningewadhili adui zao kwa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu.
(K)

Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, 
Bali wakati wao ungedumu milele.
Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, 
Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani
. (K)


SHANGILIO 
Zab. 119:34

Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.


INJILI 
Mt. 14: 13-21

Yesu aliposikia habari ya kuuawa kwa Yohane Mbatizaji, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka miiini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu. akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.

Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi kula. Wakamwambia, Hatuna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa.

Akawaagiza makutano wakati katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies