Dominika ya 26 ya Mwaka A:Kila mtu anahukumiwa kwa matendo yake

 

Dominika ya 26 ya Mwaka A:Kila mtu anahukumiwa kwa matendo yake

Tunalolisema lilingane na tunalolifikiria na tutimize kwa matendo yale tunayosema kwa maneno.Tukisema Ndiyo”iwe ni ndiyo na tukisema“hapana”iwe ni hapana”zaidi ya hayo yanatoka kwa ibilisi.Kumbe tunaalikwa kuishi na kutimiza ahadi zetu tunazoziweka mbele za Mungu na mbele za watu.Na ili tuweze kuwa waaminifu katika ahadi zetu tunapaswa kuwa na moyo wa sadaka na kudumu katika kutenda mema.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanaweka mkazo juu ya hukumu ya Mungu ilivyo ya haki maana kila mtu anaipata kutokana na matendo yake mwenyewe. Lakini Mungu ni mwenye huruma naye huwasamehe wale wanaokiri na kutubu makosa yao kama wimbo wa mwanzo unavyosisitiza kusema; “Ee Bwana, yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi, wala hatukuzitii amri zako, ulitukuze jina lako na kututendea sawasawa na wingi wa huruma zako” (Dan. 3:31, 29, 30, 43, 42). Ndiyo maana katika sala ya mwanzo tunasali kwa matumaini tukisema; “Ee Mungu, wewe unaonyesha enzi yako kuu hasa kwa kusamehe na kuhurumia. Utumwagilie daima neema yako, tupate kuzishiriki baraka za mbinguni sisi tunaokimbilia ahadi zako”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 18:25-28). Katika somo hili Nabii Ezekieli anakaza kusema kuwa Mungu ni mwenye haki. Hivyo hatamwadhibu mtu yeyote sababu ya dhambi za mtu/watu wengine madhalani wazazi au ndugu zake. Kila mtu atapata hukumu kadiri ya haki ya moyo wake na matendo yake. Nabii Ezekieli anatoa ujumbe huu kwa watu wa Taifa lake Israeli wakiwa utumwani Babeli kwamba sababu ya wao kuwa utumwani ni dhambi zao wenyewe wala si za mtu mwingine, maana wao walifikiri kuwa walipelekwa utumwani kutumikia adhabu ya dhambi za babu zao. Namna hii ya kifikiri ilisababishwa na mfumo wa kutoa adhabu katika agano la kale zilizotolewa siyo tu kwa aliyekosa bali hata kwa familia nzima, ukoo au taifa zima kuwajibishwa. Wazazi walipaswa kulipa kwa dhambi za watoto wao na watoto kwa dhambi za wazazi wao. Sheria hii ya kosa la pamoja ilikuwa maarufu katika mataifa mbalimbali ya mashariki ya mbali na Musa aliichukua na kuiingiza katika sheria za waisraeli. Tusoma hivi katika kitabu cha kutoka: “Mimi Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu na naadhibu makosa ya wazee kwa watoto wao na wajukuu kwa watoto wa wajukuu wa wale wanaonichukia” (Kut. 20:5). Lengo la Musa kuichukua sheria hii na kuifanya kama sheria ya Mungu ilikuwa ni kuwaonesha watu ubaya wa dhambi ya kuabudu miungu mingine na kuwafundisha njia za Mungu wa kweli.

Kadiri Mungu alivyoendelea kujifunua na kuweka wazi mpango wake, na mtazamo wa mwandamu nao unabadilika kwa kuwa na uelewa mzuri wa Mungu. Hivyo Nabii Ezekieli akiongozwa na Roho wa Mungu anabatilisha mtazamo huu na kuwaambia kuwa Mungu ni mwenye haki, hivyo anamwadhibu kila mtu kwa dhambi zake binafsi na sio kwa dhambi za watu wengine. Kila mtu atapata hukumu kadiri ya haki ya moyo wake na matendo yake. Hivyo wazazi wasiadhibiwe kwa sababu ya dhambi ya watoto wao, wala watoto wasiadhibiwe kutokana na dhambi za wazazi wao; kila mmoja ahukumiwe kwa dhambi zake mwenyewe. Mitume nao walikuwa na mawazo haya ndiyo maana walimuuliza Yesu kuhusu habari za mtu kuzaliwa kipofu wakisema; “Bwana ni nani aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake kwa yeye kuzaliwa kipofu?” (Yoh 9:2). Yesu aliwajibu kuwa; “Siyo yeye wala wazazi wake waliotenda dhambi; alizaliwa kipofu ili kazi ya Mungu ionekane kwa njia yake” (Yoh 9:3).

Huu ni ujumbe wa matumaini kwa wote ndio maana mzaburi alitafakari na kuomba hivi kwa maneno ya wimbo wa katikati; “Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako; uniongoze katika kweli yako na kunifundisha: maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, maana zimekuwako tokea zamani. Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, wala maasi yangu, unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. Maana wewe Bwana u mwema, mwenye adili, kwa hiyo utawafundisha njia wenye dhambi, wenye upole utawaongoza katika njia zako” (Zab. 25: 4-9). Na haya ndiyo matumaini yetu kuwa daima Mungu anatufundisha njia zake na tunapokosea kwa kutozifuata, tukakiri na kuomba msamaha anatusamehe.

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Filp 2:1-11). Somo hili limegawanyika katika sehemu kuu mbili. Katika sehemu ya kwanza mtume Paulo anatuasa tuwe na nia moja na anatuonya tusiishi kwa ugomvi wala majivuno. Tukiwa na unyenyekevu tutashinda majivuno na mafarakano na hivi tutakuwa na amani, umoja na maelewano. Katika sehemu ya pili Mtume Paulo anatualika tuufuate mfano wa Yesu Kristo aliyejinyenyekeza akawa mtii hata kufa msalabani ili kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Bwana wetu Yesu Kristo alionyesha mfano kamili wa unyenyekevu kwa kutwaa mwili wa kibinadamu, kutii, kuteswa na kufa msalabani, ili sisi tupate kukombolewa. Baada ya kujinyenyekesha hivyo Mungu alimtukuzwa na kumkweza juu kabisa katika utukufu wake. Hivyo tunaalikwa kuufuata mfano wake kwa maneno na matendo ili kwayo nasi tuweze kutukuzwa na kuweka juu mbinguni.

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 21:28-32). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anasisitiza kuwa katika kuutafuta ufalme wa Mungu ni lazima maneno na matendo yetu yaendane yakiongozwa kwa moyo wa utii na unyenyekevu. Ujumbe huu anaueleza kwa mfano wa watoto wawili wote wakionyesha ukaidi kwa baba yao kila mmoja kwa namna yake. Mtoto wa kwanza hakutimiza kabisa alichoambiwa na baba yake licha ya kuwa aliitikia kwa maneno kuwa angefanya aliyoagizwa na wa pili licha ya kumjibu vibaya baba yake kuwa hataki kufanya kazi, baadae alijirudi na mtimiza alichombiwa. Mtoto wa kwanza ni mfano wa wakristo ambao ukristo wao ni wakutimiza tu ibada na kusema nasadiki lakini matendo yao ni kinyume kabisa na imani yao. Kama Yesu mwenyewe anavyosema; “Mbona mnaniita Bwana, Bwana, lakini hamtimizi ninayowaambia?” (Luka 6:46). Kama anavyosema mtume Yakobo kuwa Imani bila matendo imekufa (Yak 2:14-26), kusadiki tu bila kuiishi hakutustahilishi kuingia Mbinguni kama Yesu mwenyewe alivyosema; “Si wote waniitao Bwana, Bwana, watakaoingia katika ufalme wa Mungu, bali ni wale wanaotimiza mapenzi ya Baba yangu” (Mt. 7:21).

Kumbe basi tujitahidi kuufanya ukristo wetu usiwe tu namna ya kusali bali uwe namna ya kuishi. Imani yetu ionekane katika namna tunavyoishi na kutenda katika familia na jumuiya zetu, tunavyoendesha shughuli za kila siku iwe ni siasi au biashara kwa kutimiza ahadi zetu na kutokuwa waongo. Mtoto wa kwanza ni mfano wa watu wanaotoa ahadi za uongo na kukosa uaminifu. Je? Sisi katika maisha yetu hatuko kama yeye? Kama wanasiasa hatutoi ahadi za uongo kwa wananchi hasa nyakati za uchaguzi ambazo tunajua kabisa hatutazitimiza? Je, hatuishi kinafiki mbele za viongozi wakubwa kwa kusema ndiyo, ndiyo, lakini kwa ndani haturidhishwi, wala hatukubaliani na hivyo hatutimizi tunayoyatamka na kuyakubali kwa midomo yetu? Huku ni kuwa na sura mbili sio wa moto wala si wa baridi bali uvuguvugu ambao ni hatari kwa maisha. Tupo wale ambao tunalolifikiria na kupanga kulitenda ni tofauti na tunalolisema; tunalolisema ni tofauti na tunalolitenda. Tunapaswa kuwa watu wa kweli, tutoe ahadi za kweli na tunazoweza kuzitimiza. Tujitahidi kuwa watu wa kuisema kweli na kuishuhudia. Tunalolisema lilingane na tunalolifikiria na tutimize kwa matendo yale tunayosema kwa maneno. Tukisema “Ndiyo” iwe ni ndiyo na tukisema “hapana” iwe ni hapana” zaidi ya hayo yanatoka kwa ibilisi. Kumbe tunaalikwa kuishi na kutimiza ahadi zetu tunazoziweka mbele za Mungu na mbele za watu. Na ili tuweze kuwa waaminifu katika ahadi zetu tunapaswa kuwa na moyo wa sadaka na kudumu katika kutenda mema.

Mtoto wa pili katika injili ni mfano wa kuwa na moyo wa toba na kuanza maisha mapya. Inawezekana wapo tunaoishi maisha yasiyofaa, maisha ya dhambi. Tusikate tamaa bali tupige moyo konde, tutubu na kumrudi Mungu naye atatusamehe na kututakasa na uovu wetu wote maana Yeye anasema; “Mtu mwovu akiighairi njia yake mbaya na kuanza kutenda mema, maovu yake yote aliyotenda hapo zamani hakuna hata moja litakalokumbukwa”. Tuige mfano wa Mtume Paulo na kusema; “Ninachokifanya, nikusahau yote ya zamani na kuchuchumilia yale yajayo” (Flp. 3:13). “Kwa sababu ya kale yote yamepita, tazama sasa yamekuwa mapya” (2Kor 5:17). Hii inatufundisha na sisi kuwa tayari kuwasamehe na kuwapokea waliotukosea wanapoomba msamaha. Hivyo tutaweza kuimba vyema antifona ya wimbo wa komonio kwa furaha tukisema; “Katika hili tumelifahamu pendo la Mungu, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” (1Yoh. 3:16).

Basi tujitahidi kudumu katika kutenda mema. Kama waswahili wanavyosema: “Usiache mbachao kwa msala upitao”, nasi tukumbuke ujumbe huu wa Mungu kwa kinywa cha Nabii Ezekieli kuwa; “Mwenye haki akiacha njia yake njema akatenda uovu, yale mazuri aliyotenda zamani hayatakumbukwa; na katika uovu wake atakufa”. Kumbe tusikubali chochote kibaya kifute wema wetu na kujitenga na upendo wa Kristo maana hakuna kitu chochote kinachozidi thamani ya upendo wa Kristo hata kitutenge nao (Rum 8:35). Tuwe makini ili maneno haya ya Mtume Paulo kwa kwa Wagalatia akisema; “Enyi Wagalatia wajinga, ni nani aliyewaloga? Mlianza katika Roho sasa mnamalizia katika mwili” (Gal 3:1), yasije tuhusu na sisi yatupasa tudumu katika kutenda mema katika roho na kweli. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa unyenyekevu na utii ili tuwe waaminifu na kutimiza ahadi zetu za Ubatizo tulizozitoa kwake na zile tulizowaahidi binadamu wenzetu na pale tunapokosea, tuwe wepesi wa kuomba msamaha, kufanya toba na kuanza upya. Na hivyo sala ya kuombea dhabihu inayosema; “Ee Mungu mwenye huruma, ukubali dhabihu yetu hii ikupendeze, nayo itufungulie chemchemi ya baraka zote” itazaa matunda ya wokovu wa kweli ndani mwetu ambayo sala baada ya komunyo inayasisitiza ikisema; “Ee Bwana, fumbo hili la mbinguni lituponye mwili na roho, tupate kuurithi utukufu pamoja na Mkombozi, ambaye tunamsikitikia tunapohubiri kufa kwake”

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies