MAFUNDISHO JUU YA ROHO MTAKATIFU NDANI YA KANISA KATOLIKI

 

Nini maana ya Roho Mtakatifu?

Roho Mtakatifu ni nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu, ni Mungu Halisi sawa na Mungu Baba na Mwana. (Yoh 14:16-17,26)

Roho Mtakatifu ni nani?
Roho Mtakatifu ni upendo wa Mungu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, mwenye Umungu mmoja na Baba na Mwana.
“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5).
Ametumwa kwetu atufanyie kazi pasipo kuonekana.
“Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh 3:8).
“Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Rom 8:14).

Je, kazi zote za Roho Mtakatifu zinahusiana na Yesu?
Ndiyo, kazi zote za Roho Mtakatifu zinahusiana na Yesu na kulenga hasa kuandaa watu wampokee, wamfuate na kumshuhudia katika umoja wa kundi lake, Kanisa.
“Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia” (Yoh 15:26-27).

Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni lipi?
Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni umoja wa Kanisa unaotokana na ustawi wa upendo na vipaji ndani ya waamini.
“Wote walijaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:31-32).
“Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” (Gal 5:22-23).
“Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi; tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki” (Yak 3:14-17).

Roho Mtakatifu anatusaidiaje kusali?
Roho Mtakatifu anatusaidia tusali kama Yesu, akiwa mlezi wa ndani na kutumia vipaji vyake saba.
“Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Gal 4:6).
“Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa… huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu” (Rom 8:26-27).
Ndiyo sababu Kanisa linatuhimiza tumtamani na kumualika kila mara, ‘Njoo, Roho Mtakatifu!’ yaani kumuomba Baba kwa njia ya Mwana amtume zaidi na zaidi ndani mwetu.


No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies