MASOMO YA MISA, JUMANNE , SEPTEMBA 5, 2023 JUMA LA 22 LA MWAKA


MASOMO YA MISA, JUMANNE , SEPTEMBA 5, 2023
JUMA LA 22 LA MWAKA

Kumbukumbu ya Mtakatifu Teresia wa Kolkota

SOMO 1
1The. 5:1-6, 9-1
Ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna Amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 27:1,4, 13-14 (K) 13

(K) Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai.

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)

Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana,
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana,
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SHANGILIO
2Tim. 1:10

Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti,
na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.

INJILI
Lk. 4:31 – 37
Yesu alishuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya sabato; wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo.
Na ndani ya sinagogi mlikuwa na mtu mwenye roho ya pepo mchafu, akalia kwa sauti kuu, akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno. Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, Ni neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka. Habari zake zikaenea kila mahali katika nchi ile.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies