MASOMO YA MISA,
JUMAPILI, SEPTEMBA 3, 2023
JUMA LA 22 LA MWAKA
MWANZO
Zab. 86:3, 5
Ee Bwana, unifadhili maana nakulilia wewe mchana kutwa. Kwa maana wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao.
SOMO I
Jer. 20:7-9
Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki. Maana kila ninenapo napiga kelele; nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja wala sitasema tena kwa jina lake; ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 63:1-5, 7-8 (K) 1
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.
Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu.
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na chovu, isiyo na maji. (K)
Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai,
Midomo yangu itakusifu. (K)
Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai,
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono,
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. (K)
Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu imekuandama sana,
SOMO 2
Rum 12: 1-2
Basi ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Lk 21: 36
Aleluya, aleluya,
Kesheni kila wakati, ili mpate kuokoka,
na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.
Aleluya
INJILI
Mt 16:21-27
Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema. Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.
Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayeipoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
No comments
Post a Comment