MASOMO YA MISA, JUMATANO, SEPTEMBA 6, 2023


JUMA LA 22 LA MWAKA 
________

SOMO I
Kol. 1:1-8

Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu, kwa ndugu watakatifu, waminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na Amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu.

Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, sikuzote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za Imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokuwa kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 52:8-9 (K) 8

(K) Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.

Mimi ni kama mzeituni,
Umeao katika nyumba ya Mungu.
Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele. (K)

Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; 
Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema;
Mbele ya wacha Mungu wako. (K)
________

SHANGILIO
Yak. 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, 
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, 
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya
________

INJILI
Lk. 4:38 – 44

Yesu alitoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia.

Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.

Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafutatafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies