MASOMO YA MISA, JUMATATU, SEPTEMBA 4, 2023
SOMO I
1 Thes. 4:13-17
Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1, 3-5, 11-13 (K) 13
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi zote.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana.
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu,
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. (K)
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya
INJILI
Lk. 4:16 – 30
Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.
Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake.
Wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende hapa pia katika nchi yako mwenyewe. akasema, Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubalika nchi yake mwenyewe.
Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitano na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.
Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
No comments
Post a Comment