Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Tumaini na Far...

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Tumaini na Faraja Kwa Kanisa Linalosafiri
  Sherehe hii ya Kupalizwa Mbinguni Mama Bikira Maria, haipatika

ni moja kwa moja kwenye Maandiko Matakatifu, bali ni matunda ya Mapokeo ya Kanisa ambayo ni Mahubiri ya Mitume, Mababa wa Kanisa na Imani ya Wakristo wa kwanza, lakini msingi wake umo ndani ya Maandiko Matakatifu na tunaalikwa daima kuyaamini mafundisho haya na kuyaishi kwa sababu Mapokeo pia ni moja ya hazina ya Neno la Mungu pamoja na Maandiko Matakatifu: Bikira Maria: Tumaini!

Na Padre Michael Lusato - Roma

Utangulizi: Tafakari ya Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria: Bikira Maria ni ishara na tumaini thabiti na ya faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri. Tunaposherehekea Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Mama Bikira Maria, tunajifunza kuwa, Mama wa Yesu, akiwa amekwisha tukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa Taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja (taz. 2Pet 3:10; Lumen Gentium, n. 68). Somo la kwanza: Ufunuo 11-.19; 12:1-6.10. Somo la pili: 1 Wakorinto 15:20-26. Injili: Luka 1:39-56. Karibu mpenzi msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari hii, leo ambapo Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Mama Bikira Maria Mtakatifu. Sherehe hii ya Kupalizwa Mbinguni Mama Bikira Maria, haipatikani moja kwa moja kwenye Maandiko Matakatifu, bali ni matunda ya Mapokeo ya Kanisa ambayo ni Mahubiri ya Mitume, Mababa wa Kanisa na Imani ya Wakristo wa kwanza, lakini msingi wake umo ndani ya Maandiko Matakatifu na tunaalikwa daima kuyaamini mafundisho haya na kuyaishi kwa sababu Mapokeo pia ni moja ya hazina ya Neno la Mungu pamoja na Maandiko Matakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya Dei Verbum, n. 8 wanasema: “Kwa hiyo, mahubiri ya kitume, yanapatikana kwa namna ya pekee katika Vitabu Vitakatifu, ilikuwa lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa mfululizo wa kupokezana mpaka mwisho wa nyakati. Hivyo basi, Mitume, wanapowarithisha wengine yale waliyopokea, wanawasihi waamini wahifadhi Mapokeo waliyopewa ama kwa maneno au kwa maandishi (taz. 2The 2:15). Na pia waliwasihi wapiganie imani waliyopewa mara moja tu na kwa daima (taz. Yda 1:3). Yale ambayo Mitume waliyarithisha, ndani yake yamo yote yenye kulifanya Taifa la Mungu kuishi katika utakatifu na kukuza imani yake. Hivyo Kanisa, katika mafundisho yake na katika maisha na ibada zake, linaendeleza daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na pia juu ya yale anayoyaamini.”

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Fajana matumaini

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya Dei Verbum, n. 9 wanaendelea kusema: “Kwa hiyo Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yameshikamana pamoja na kushirikiana. Kwa sababu yote mawili yanabubujika kutoka katika chemchemi ileile ya kimungu na hivyo huungana na kuwa kitu kimoja na kuelekea lengo moja. Kwa kweli, Maandiko Matakatifu ndilo Neno la Mungu ambalo liliandikwa kwa uvuvio wa Roho wa Mungu. Neno la Mungu lililokabidhiwa kwa Mitume na Kristo Bwana na Roho Mtakatifu linarithishwa li zima na Mapokeo Matakatifu kwa waandamizi wao, ili, wakiangazwa na Roho wa kweli, kwa njia ya kuhubiri kwao, walihifadhi kiaminifu, walifafanue na kulieneza. Hivyo Kanisa halichoti uhakika wake juu ya mambo yote yaliyofunuliwa kutokana na Maandiko Matakatifu peke yake. Kwa hiyo Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu lazima yapokelewe na kuheshimiwa kwa hisia sawa, za uchaji na heshima.” Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kusema, katika Hati ya Dei Verbum, n. 10 kwamba: “Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yanaunda hazina moja takatifu ya Neno la Mungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Taifa lote takatifu pamoja na Wachungaji wake likishikamana na hazina hiyo, linadumu daima aminifu katika Mafundisho ya Mitume na katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali (taz. Mdo 2:42), ili, katika kuitunza, kuiishi na kuikiri imani iliyorithishwa, uwepo umoja wa pekee wa kiroho kati ya Maaskofu na waamini.”

Bikira Maria ni faraja na matumaini ya Kanisa linalosafiri hapa duniani

Tafakari: Moja ya mafundisho haya ya Kanisa ni kutoka katika somo la kwanza tulilosikia, kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohane 11:19; 12:1-6.10. Katika somo hili, Mababa wa Kanisa wanafundisha kuwa, kwanza somo linazungumzia mwanamke ambaye ni sura ya taifa la Mungu, ambalo ndilo Kanisa, ambapo pia Maria anawakilisha sura ya taifa la Mungu yaani Kanisa. Simulizi hili la joka linaturudisha kwenye kitabu cha Mwanza 3:15 ambapo Mungu aliweka uadui kati ya mwanamke na nyoka na kati ya uzao wa mwanamke na uzao wa nyoka ambaye ni shetani. Mwanamke aliyevikwa jua. Hii ni ishara ya kuwa mwanamke huyu amepambwa kwa neema za Mungu (salamu uliye jaa neema – salamu ya Malaika Gabrieli kwa Bikira Maria). Na mwezi chini ya miguu yake, maana yake kuwa mwanamke huyu hatapotea wala kuamgamia, bali ataishi milele. Na juu ya kichwa chake taji ya nyota 12, zinazowakilisha makabila 12 ya wana wa Israeli. Pia huwakilisha Mitume 12 ya Yesu, ikiwa na maana ya utawala wa Kanisa katika ulimwengu. Naye alikuwa na mimba akilia hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. Hii li lugha ya picha inayoonesha mateso ya wokovu yaliyoletwa au kutimizwa na Kristo pale msalabani na hatimaye kufufuka kwa ushindi. Naye akazaa mtoto wa kiume – huyu ndiye Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu, na mtoto huyu akanyakuliwa hata kwa Mungu, picha ya mateso, kifo, ufufuko na kupaa mbinguni kwa Kristo. Mwanamke akakimbilia nyikani, hii huwakilisha ukimbizi wa Wakristo wa kwanza kwa sababu ya mateso. Kusudi tuweze kutafakari vizuri Sherehe hii, lazima tuanze kwenye simulizi la uumbaji wa mwanadamu. Tunaambiwa kwamba Mungu alimuumba mwanaume kutoka katika mavumbi kisha akampulizia puani pumzi ya uhai (rej. Mwanzo 2:6 - 7).

Bikira Maria Amepalizwa Mbinguni Mwili na Roho

Mungu alimuumba mtu akiwa mwili na roho. Haukuwa mpango wa Mungu kwamba mwili na roho vitengane. Utengano wa mwili na roho ni matokeo ya dhambi ya Adam na Eva. Baada ya kosa la Adam na Eva, Mungu alitoa adhabu kwa nyoka, mwanamke na mwanaume (rej. Mwanzo 3: 14-19). Moja ya adhabu iliyotolewa ni mwanadamu kurudi mavumbini alikotwaliwa. Bikira Maria kwa mujibu wa imani Katoliki amekingwa na dhambi ya asili hivyo hakuna ajabu tunapoambiwa amepalizwa mbinguni. Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria maana yake ni kwamba, alichukuliwa mbinguni mwili na roho. Yeye ambaye hakurithi dhambi ya asili alikingwa pia na matokeo ya dhambi hiyo. Hakurudi mavumbini. Kwa sababu alijitoa mzima bila kujibakiza katika kutimiza mapenzi ya Mungu, yaani kuwa Mama wa Mungu, na hivyo kujiweka chini ya mapenzi ya Mungu na kutii ili Mungu atimize kile alichopanga yaani ukombozi wa mwanadamu kupitia kwake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya Lumen Gentium, n. 59 wananasema: “Mwishowe, Bikira asiye na doa, aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni pamoja na mwili [wake] na pamoja na roho [yake]; akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, ili afananishwe kikamilifu zaidi na Mwanawe, aliye Bwana wa mabwana (taz. Ufu 19:16) na mshindi wa dhambi na mauti.” Kupalizwa mbinguni kwa Bikira Maria pia kunatukumbusha fundisho la Mtakatifu Agustino kwamba kila alichonacho Yesu kwa asili yake kama Mungu, Maria amejaliwa kwa neema. Yesu kwa asili yake kama Mungu asingeweza kufungwa kaburini. Alifufuka na kupaa mbinguni mwili na roho. Vivyo hivyo, Bikira Maria kwa neema anachukuliwa mbinguni mwili na roho kwa sababu alishiriki kikamilifu katika ukombozi wa mwanadamu – kazi iliyomleta Kristo duniani.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila

Mtakatifu Yohane wa Damasko anasema: Ilifaa kwamba yeye, ambaye alikuwa ameutunza ubikira wake katika kuzaa, auweke mwili wake bila uharibifu wowote hata baada ya kifo. Ilifaa kwamba yeye, ambaye alikuwa amembeba Muumba kama mtoto kwenye kifua chake, anapaswa kukaa ndani ya tabernakulo za kimungu. Ilifaa kwamba bi harusi, ambaye Baba alimchukua kwake, aishi katika makao ya kimungu. Ilifaa kwamba yeye, ambaye alikuwa amemwona Mwanawe juu ya msalaba na ambaye kwa njia hiyo alikuwa amepokea moyoni mwake upanga wa huzuni ambao aliukimbia katika tendo la kumzaa, inatakiwa kumtazama akiwa amekaa na Baba. Ilifaa kwamba Mama wa Mungu amiliki kilicho cha Mwanawe, na aheshimiwe na kila kiumbe kama Mama na mjakazi wa Mungu. Bikira Maria ni kazi bora zaidi ya uumbaji iliyofanywa na Mungu Baba. Bikira Maria ni kiumbe mkamilifu kabisa. Mungu anapoumba watu kuna namna au kusudio la anavyotaka watu hao aliowaumba wawe. Hakuna hata mtu mmoja zaidi ya Bikira Maria (ukiacha Yesu) ambaye amekuwa kwa asilimia mia moja vile vile Mungu alivyotaka awe. Wengine wote tumekuwa pungufu ya kile Mungu alichotaka. Kama Bikira Maria ni kiumbe bora hivyo sio ajabu kabisa kuwa Mungu Baba hakutaka kazi yake bora na ya ajabu ambayo Mungu mwenyewe anaistaajabia iozee kaburini. Anampokea binti yake mpendwa mbinguni akiwa mwili na roho. Ndio kusema kwamba, baada ya Mungu kumpa Bikira Maria zawadi kubwa kuliko zote, yaani ya kuwa Mama wa Mungu, sasa anamuinua mbinguni ili ashiriki matunda ya Mwana.

Miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu

Yesu aliye Nafsi ya pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu alipata mwili wake kutoka kwa Bikira Maria. Kama vile Adam alivyomwangalia Eva na kusema huyu ni mifupa katika mifupa yangu na nyama katika nyama yangu (rej. Mwanzo 2: 23), Yesu pia akimtazama Maria anaweza kutamka maneno hayo ya Adamu wa kwanza kwa njia ya “analojia.” Katika hali hii haishangazi Yesu kuzuia mwili ule uliomtengeneza Yeye usiozee kaburini na akaupokea mbinguni. Bikira Maria amekuwa mwaminifu kwa Roho Mtakatifu na malipo ya uaminifu wake ni kuaminiwa na Mungu Roho Mtakatifu kiasi cha kumfanya awe chombo chake cha neema zote. Kama ilivyo kwenye tukio la Yesu kupaa mbinguni, hili la Bikira Maria kupalizwa mbinguni linatufundisha kuwa kuna maisha ng’ambo ya kaburi. Na kwamba mwanadamu kamili ni mwili na roho. Mungu anathamini yote mawili. Miili yetu ni hekalu ya Roho Mtakatifu na ni mpango wa Mungu siku ya mwisho wote twende mbinguni mwili na roho. Tutapewa miili ya utukufu. Watakatifu walioko mbinguni wako katika hali ya ukamilifu lakini Bikira Maria ameshafikia ukamilifu timilifu. Watakatifu wengine wataungana mwili na roho baada ya hukumu ya mwisho lakini Bikira Maria tayari yuko katika hali hiyo ya utimilifu. Hivyo tunapomtafakari yeye aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, tunaona zikifunguliwa kwetu zile “mbingu mpya” na “nchi mpya” ambazo zitatokea wakati wa kuja kwa Kristo mara ya pili. Bikira Maria amepalizwa mbinguni ili pia kupokea tuzo. Bikira Maria aliteseka na Yesu. Baada ya Msalaba sasa ni utukufu na kabla ya utukufu ilikuwa Msalaba! Kwa maneno mengine Bikira Maria alikufa kiroho pamoja na Yesu pale Msalabani baada ya kujitoa mzima kushiriki katika mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu. Maria Mama wa Mateso ya Kalvari sasa anafurahia utukufu wa Mwanae. Hivyo tunapojifunza kuteseka na kufa kama Maria na pamoja na Maria hatutakuwa na wasiwasi ya nini kitatokea baadaye, kwa sababu Mungu mwenyewe atatimiza ahadi yake ya kutufanya tuketi pamoja na Kristo na Maria katika utukufu wake. Hii inatupa faraja kwamba kama tutavumilia magumu ya ulimwengu huu, siku moja tutafaidi pia faraja ya mbinguni. Kwamba mwisho wa yote mauti itashindwa na uzima utashinda.

Bikira Maria Aliyepalizwa mbinguni ni kielelezo cha huduma ya upendo

Tukiangalia Injili ya leo (Luka 1:39-56) simulizi la Bikira Maria kwenda kumtembelea Elizabeti. Malaika alipomwambia Maria kuwa atapata ujauzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, alimfahamisha pia kuwa Elizabeti aliye shangazi wa Maria naye ana ujauzito wa miezi sita. Miujiza miwili; tasa amepata mimba na bikira naye kapata pia ujauzito. Malaika alimwambia Maria hakuna kisichowezekana kwa Mungu. Mungu hafungwi na sheria za maumbile. Uwezo wa Mungu unazidi upeo wa ufahamu wetu wa kibinadamu. Malaika anapoondoka Bikira Maria anaondoka kwa haraka kwenda kwa Elizabeti. Katika safari hii ya Maria, Roho Mtakatifu kwa kinywa cha Elizabeti anatangaza sifa za Bikira Maria. Anamtangaza Maria kuwa Mama wa Mungu. Elizabeti anaposema "limenitokeaje neno hili hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?" (rej. Lk 1:43). Neno "Bwana" limesimama kwa maana ya "Mungu". Elizabeti anatutangazia kuwa Maria ni Mama wa Bwana au Mama wa Mungu. Sifa nyingine inayotangazwa katika tukio hili ni namna Bikira Maria alivyobarikiwa. Elizabeti anasema; "Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote." (rej. Lk 1:41-42). Tukumbuke maneno haya Elizabeti aliyasema akiwa amejaa Roho Mtakatifu kwa hiyo sio maneno ya mropokaji. Ni kama vile Roho Mtakatifu anazungumza kupitia mdomo wa Elizabeti. Elizabeti pia anatutangazia kwamba Bikira Maria ni mwenye imani kubwa ndio maana anasema; “Naye heri aliyesadiki; maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.” (rej. Lk 1:45). Baada ya sifa hizi za Maria kushuhudiwa na Elizabeti, Maria mwenyewe anatuonesha sifa zake nyingine. Unyenyekevu. Hajisifu, bali anamsifu Mungu kwa maana anatambua kuwa yote aliyopata ni kwa upendo na huruma ya Mungu kwake na kwa wanadamu wote.

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni: Nadhiri

Tuhitimishe tafakari yetu kwa kusema kuwa tusihofu kumsifu Maria kwa sababu kila mara tunapomsifu Maria, yeye mara moja huzigeuza sifa hizo kuwa za Mungu. Ndio maana Elizabeti alipomsifu, mara moja Bikira Maria akasema “Moyo wangu wamtukuza Bwana...” Utenzi huu unaeleza hali ya kiroho ya Bikira Maria, na hakuna kitu kikubwa zaidi ya hali hii ya kiroho kwa ajili ya kutusaidia kupata uzoefu wa Fumbo la Ekaristi. Ekaristi imetolewa kwetu ili maisha yetu, kama yale ya Bikira Maria, yawe ya ukuu kabisa. Kwa maana “Mama anapoheshimiwa, Mwana hupata kujulishwa, kupendwa na kutukuzwa inavyostahili, na amri zake kushikwa, kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa (rej. Kol 1:15-16) na katika yeye ilimpendeza Baba wa milele utimilifu wote ukae (rej. Kol 1:19).” Tumtazame Bikira Maria, yeye anatufungulia matumaini ya wakati ujao uliojaa furaha na anatufundisha njia ya kuufikia: yaani kumpokea mwanaye kwa imani; daima tusipoteze urafiki wetu na mwanaye, bali tujiachilie ili, Mwanaye atuangazie mwanga wake na atuongoze kwa Neno lake; tumfuase mwanaye kila siku, hata nyakati ambazo tunahisi misalaba yetu kuwa mizito. Maria Sanduku la Agano Jipya aliye Mbinguni, anatuonesha kwa mwanga halisi kwamba tupo katika njia tukielekea katika nyumba yetu ya kweli, yaani ushirika wetu wa furaha na amani pamoja na Mungu. Hivyo, waamini wote wakristo wamsihi kwa nguvu Mama wa Mungu na Mama wa wanadamu, ili yeye aliyeusaidia mwanzo wa Kanisa kwa maombezi yake, pia sasa aliyetukuzwa mbinguni, juu ya Wenye heri na Malaika, awaombee kwa Mwanawe katika Ushirika wa Watakatifu wote, mpaka jamaa zote za Mataifa zilizopambwa jina la Kristo au zisizomjua bado Mwokozi wao, zikusanyike kwa furaha kuwa Taifa moja la Mungu katika amani na mapatano, kwa utukufu wa Utatu Mtakatifu sana usiogawanyika. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies