TAFAKARI YA MASOMO YA MISA JUMANNE SEPTEMBER 26;2023


Jumanne, Septemba 26, 2023
Juma la 25 la Mwaka

Ezra 6: 7-8,12,14-20;
Zab 121: 1-5;
Lk 8: 19-21

FAMILIA YA MUNGU!
Familia changa kwa kawaida inaonekana kuwa na umoja na mshikamono zaidi kwa mtazamo wa hapa duniani. Lakini, Yesu anatufundisha kwamba kuna uhusiano na umoja wa karibu zaidi kuliko wa familia, umoja na mshikamano alio nao kati yake na wafuasi wake. Hili ndilo fundisho tunalo pata kutoka katika Injili ya leo. Yesu alikuwa amesimama mbele ya umati wa watu akiwafundisha na mara moja ukaja ujumbe, kwamba Mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje wakitaka kumuona. Jibu lake kwao linaonekana kama anamkataa Mama yake. Haikatai familia yake na wala hakuonesha kwamba haina umuhimu, na wala hakufundisha kwamba familia ya Kibinadamu ina nafasi ndogo kwa Mungu. Yeye anatangaza kuhusu uwepo wa familia ya pekee-familia ya kiroho. Familia ya kiroho na uhusiano wake umejikita katika Neno la Mungu-kulisikia na kuliishi. Mtu aliye karibu na Mungu ni mtu anaye mtii Mungu, anaye chukulia neno lake kwa umakini.

Yesu anasema wale wanao lishika neno lake na kuliishi ndio Mama, Kaka na ndugu zake. Bikira Maria Mama yake, ndiye wakwanza kabisa kulisikia neno la Mungu na kulitenda katika ukamilifu wote, kwa hiyo unaweza kuona kwamba Yesu hakumkataa Mama yake bali alitaka sisi nasi tuwe ndugu zake kwa kuishi katika kulishika neno lake. Sisi tutakuwa ndugu wa Yesu kweli kama tutaishi kadiri ya Mafundisho yake. Tunaweza kusema tunampenda Yesu kweli kama tunashika yale aliyo tufundisha. Tusizibe masikio yetu kwa wenzetu wala kwa maskini wanapo kuwa na shida kwasababu sisi tunakuwa familia moja na Yesu na wala tusitamani uovu kwasababu kiongozi wetu hana uovu ndani yake.

Tutafakari leo kuhusu mwaliko wa Yesu wa kututaka sisi tuweze kuwa mmoja wapo wa familia yake, sema “ndio” kwa mwaliko huu. Tuwe tayari kwa sauti yake na Umungu wake utabadilisha maisha yetu.

Sala: Bwana, ninapokea mwaliko wako wa kuwa mmoja wapo wa familia yako ya karibu. Ninaomba nisikie sauti yako na niweze kutenda yale yote unayo niambia. Yesu nakuamini wewe. Amina

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies