MASOMO YA MISA 25 OCTOBER 2023

MASOMO YA MISA25 OKTOBER , 2023
JUMATANO, JUMA LA 29 LA MWAKA

SOMO 1

Rum. 6:12-18
Dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.

Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha! Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa utii uletao mauti, au kwa mba ni utumishi wa utii uletao haki. Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake; na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi mkawa watumwa wa haki.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 124 (K)

(K) Msaada wetu u katika jina la Bwana.

Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia.
Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu. (K)

Papo hapo maji yangalitudharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu;
Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu,
Maji yafurikayo.
Na ahimidiwe Bwana;
Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. (K)

Nafsi yetu imeokoka kama ndege,
Katika mtego wa wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. (K)

SHANGILIO
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI
Lk. 12:39-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.
Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.

Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies