MASOMO YA MISA 3,OCTOBER,2023

Masomo ya Misa Jumanne 03.10.2023









SOMO 1
Zek 8:20-23
Bwana wa majeshi asema hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi; wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni zetu kwa haraka tuombe fadhili za Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi nami nitakwenda. Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili za Bwana. Bwana wa majeshi asema hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.

Wimbo wa Katikati

Zab 87

Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.

Bwana ayapenda malango ya Sayuni Kuliko maskani zote za Yakobo.

Umetajwa kwa mambo matukufu, Ee Mji wa Mungu.

(K) Mungu yu pamoja nasi

Nitataja Rahabu na Babeli Miongoni mwao wanaonijua.

Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi; Huyu alizaliwa humo.

Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,

Huyu na huyu alizaliwa humo. Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara.

(K) Mungu yu pamoja nasi

Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa, Huyu alizaliwa humo.

Waimbao na wachezao na waseme, Visima vyangu vyote vimo mwako.

(K) Mungu yu pamoja nasi

Shangilio

Zab 119:105

Aleluya, Aleluya,

Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.

Aleluya.

INJILI
Lk 9:51-56
Ilikuwa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies