MASOMO YA MISA 4,OCTOBER,2023

Masomo ya Misa Jumatano  04.10.2023

SOMO 1
Neh 2:1-8
Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote. Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana. Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto? Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga. Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda. Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda; nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.

Wimbo wa Katikati

Zab 137:1-6

Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,

Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.

Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu.

(K) Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa ka kinywa changu, nisipokukumbuka.

Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie;

Na waliotuonea walitaka furaha;

Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.

(K) Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa ka kinywa changu, nisipokukumbuka.

Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,

Mkono wangu wa kuume na usahau.

(K) Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa ka kinywa changu, nisipokukumbuka.

Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu,nisipokukumbuka.

Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.

(K) Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa ka kinywa changu, nisipokukumbuka.

INJILI
Lk 9:57-62
Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata ko kote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies