MASOMO YA MISA IJUMAA 20,2023

 Mwenyeheri Bertila Boskardin, Mtawa

Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Rum 4:1-8
Tusema juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake huhesabiwa kuwa ni neema, bali kuwa na deni. Lakini kwa asiyefanya kazi, bali amwamini yeye ambaye amhesabia haki asiye mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 32:1-2, 5, 11

  1. Heri aliyesamehewa dhambi,
    Na kusitiriwa makosa yake.
    Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
    Ambaye rohoni mwake hamna hila.
    (K) Ni Wewe sitara yangu, Ee Bwana.
  2. Nalikujulisha dhambi yangu,
    Wala sikuuficha upotovu wangu.
    Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
    Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
  3. Mfurahieni Bwana;
    Shangilieni, enyi wenye haki;
    Pigeni vigelegele vya furaha;
    Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo. (K)

INJILI: Lk 12:1-7
Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari. Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa, mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

TAFAKARI:
JILINDENI NA UNAFIKI: Kristo anawafundisha makutano kuhusu maswala matatu yanayoshabihiana; kujilinda na unafiki, kutoogopa na kumwamini Mungu. Mtume Paulo anatumia mfano wa Abrahamu ili kuhimiza kuhusu zawadi ya imani kutoka kwa Mungu. Japo alijitahidi kutii na kufuata maelekezo ya Mungu, neema za Mungu kwake hazikutokana na mastahili yake kwa kutii sheria, bali yalitokana na imani yake kwa Mungu. Matendo yake yalikuwa ni ibada kamili kwa alichokiamini. Hata kama alitii, hakujiona kuwa anayestahili lolote kutoka kwa Mungu. Mwanadamu asisahau kwamba hata kama anatii sheria za Mungu, hana madai ya kufanya mbele za Mungu. Mahusiano ya Mungu na mwanadamu siyo mahusiano ya mtu na mfanyakazi wake, hivi kwamba akimaliza kazi aliyopewa anadai mshahara. Mwanadamu asisahau kwamba yeye mwenyewe na kila alicho nacho ni mali ya Mungu. Hata hivyo haina maana kwamba matendo ya mwanadamu hayana umuhimu wake. Imani inamwelekeza mtu kujituma katika matendo ya upendo. Hata baada ya kutimiza yote, tunasubiria kutoka kwa Mungu kana kwamba hatukustahili chochote.

SALA: Tupe nguvu ya kutenda yatupasayo na kusubiria kipaji cha ya neema zako. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies