MASOMO YA MISA JUMATATU, OKTOBA 16, 2023


JUMATATU, OKTOBA 16, 2023

JUMA LA 28 LA MWAKA 
________
SOMO I
Rum. 1:1-7

Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa Imani, kwa ajili ya jina lake; ambao kaitka hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na Amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 98:1-4
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. 
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. 
Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. 
________
SHANGILIO
Zab. 119:34
Aleluya, aleluya,
Unifahamishe name nitaishika sheria yako,
nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.
________
INJILI 
Lk. 11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies