MASOMO YA MISA OCTOBER 31,2023


SOMO 1
Rum. 8; 18-25
Nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibufu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K) 3

(K) Bwana alitutendea mambo makuu.

Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)

Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)

Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)

Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Alichukuapo miganda yake. (K)

SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.

INJILI
Lk. 13:18-21
Yesu alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punji ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.

Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pichi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.



No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies