MASOMO YA MISA OCTOBER 7,2023

Masomo ya Misa Jumamosi 07.10.2023

SOMO 1
Bar 4:5-12, 27-29
Jipeni moyo watu wangu, Israeli mnaokumbukwa! Mliuzwa kwa mataifa lakini hamkuangamia. Kwa kuwa mlimtia Mungu ghadhabu mlitolewa kwa adui zenu; Mlimwasi yeye aliyewaumba, mkitoa sadaka kwa pepo, si kwa Mungu; mlimsahau Mungu wa milele aliyewalea, na Yerusalemu mama yenu. Huyu mama aliiona ghadhabu ya Mungu iliyokuja juu yenu, akasema: Enyi wa Sayuni, sikilizeni! Mungu ameleta juu yangu huzuni kubwa. Nimeuona utumwa wa wanangu ambao Aliye wa Milele amewapatiliza. Kwa furaha naliwalea; bali kwa kilio na maombolezo naliwaaga. Asisimange juu yangu mtu ye yote, mimi niliye mjane na kuachwa na watu. Kwa sababu ya dhambi za wanangu nimeachwa ukiwa, kwa kuwa walikengeuka na kuiacha sheria ya Mungu.Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu! Maana yeye aliwapatiliza mambo haya atawakumbuka. Kama ilivyokuwa nia yenu kumwasi Mungu, rudini sasa, mtafuteni mara kumi zaidi; maana yeye aliyeyaleta mapigo haya juu yenu atawarudishia Furaha ya milele pamoja na wokovu wenu.

Wimbo wa Katikati

Zab 69:32-36

Walioonewa watakapoona watafurahi;

Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,

Wala hawadharau wafungwa wake.

Mbingu na nchi zimsifu,

Bahari na vyote viendavyo ndani yake.

(K) Bwana huwasikia wahitaji.

Maana Mungu ataiokoa Sayuni,

na kuijenga miji ya Yuda,

Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.

Wazao wa watumishi wake watairithi,

Nao walipendao jina lake watakaa humo.

(K) Bwana huwasikia wahitaji.

INJILI
Lk 10:17-24
Wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies