MASOMO YA MISA OKTOBA 23, 2023

JUMATATU, JUMA LA 29 LA MWAKA



SOMO 1
Rum. 4: 20-25

Ibrahimu akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa Imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoadhidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki. Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi tuatakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makossa yetu, na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

________

WIMBO WA KATIKATI
Lk. 1:69-75 (K)

(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli.

Ametusimamishia pembe ya wokovu.
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu. (K)

Tuokolewe na adui zetu,
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu. (K)

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki,
Mbele zake siku zetu zote. (K)
________

SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.
________

INJILI
Lk. 12;13-21

Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.

Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies