MASOMO YA MISA NOVEMBER 10,2023




MASOMO YA MISA IJUMAA 10,NOVEMBER 2023

SOMO 1
Rum. 15:14-21

Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba ninawakumbusha,, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.
Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu Mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1-4 (K) 2

(K) Bwana ameufunua wokovu wake.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtenda wokovu. (K)

Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

SHANGILIO
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema, mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI

Lk. 16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies