MASOMO YA MISA NOVEMBER 1,2023

MASOMO YA MISA, NOVEMBER 1, 2023

JUMATANO, JUMA LA 30 LA MWAKA

SHEREHE YA WATAKATIFU WOTE

SOMO 1
Ufu. 7:2-4,9-14
Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu.

Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-kondoo.
Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa aliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 24:1-6 (K) 6

(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. (K)

Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)

Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

SOMO 2
1 Yoh. 3:1-3
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa; kama yeye alivyo mtakatifu.

SHANGILIO
Mt. 11:28

Aleuya, aleluya.
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa
na mizigo, nami nitawapumzisha, asema Bwana.
Aleluya.

INJILI
Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjua; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.
Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies