ALHAMISI KUU MISA YA JIONI

 MASOMO MISA YA KRISIMA

ALHAMISI KUU MISA YA JIONI

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Gal.6:14

Lakini sisi yatupasa kuona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndani yake mna wokovu, uzima na ufufuko wetu, nasi tumeokolewa na kusalimishwa naye.



KOLEKTA:

Ee Mungu, tumekusanyika ili kuadhimisha Karamu takatifu sana ambamo Mwanao, kabla ya kutolewa afe, alilikabidhi Kanisa kwa karne zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake. Tunakuomba utujalie, tupate kuchota katika fumbo hili kuu utimilifu wa mapendo na uzima. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu milele na milele.


SOMO 1: Kut.12:1-8,11-14

Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi za Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwanakondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwanakondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwanakondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwanakondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu, kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwanakondoo. Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi: mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.116:12-13,15-18

1. Nimrudishie Bwana nini

Kwa ukarimu wake wote alionitendea?

Nitakipokea kikombe cha wokovu;

Na kulitangaza jina la Bwana.


(K) Kikombe kile cha Baraka tukibarikicho, Je! Si ushirika wa damu ya Kristo?


2. Ina thamani machoni pa Bwana,

Mauti ya wacha Mungu wake.

Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,

Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako.

Umevifungua vifungo vyangu. (K)


3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;

Na kulitangaza jina la Bwana;

Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,

Naam, mbele ya watu wake wote. (K)


SOMO 2: 1Kor.11:23-26

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akikitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.


SHANGILIO: Yn.13:34

Amri mpya nawapa, Mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi, asema Bwana.

INJILI: Yn.13:1-15

Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye aliwapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni, naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na yakuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuteti tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:

Ee Bwana, tunakuomba utujalie kushiriki kwa heshima mafumbo haya, kwani, kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka. Tunaomba haya kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI

Sadaka na sakramenti ya Kristo

K. Bwana awe nanyi.

W. Na awe rohoni mwako.

K. Inueni mioyo.

W. Tumeiinua kwa Bwana.

K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.

W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Yeye aliye Kuhani wa kweli na wa milele, alipoweka utaratibu wa sadaka hii ya kudumu alijitoa wa kwanza kwako kafara ya kuleta wokovu akatuagiza na sisi tuitoe kwa kumkumbuka Yeye.

Nasi tunaimarishwa, tupokeapo mwili wake uliotolewa sadaka kwa ajili yetu, na tunatakaswa tuinywapo damu yake iliyomwagika kwa ajili yetu.

Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho.

Mtakatifu, Mtakatifu,Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.11:24-25

Huu ndio Mwili wangu ulio kwa ajili yenu. Kikombe hiki ni agano jipya katika Damu yangu, asema Bwana. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:

Ee Mungu mwenyezi, kama vile tunavyotiwa nguvu na Karamu ya Mwanao hapa duniani, vivyo hivyo utujalie tustahili kushiba katika karamu ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies