IJUMAA KUU MWAKA 2024 :KATIKA MATESO YA BWANA

 IJUMAA KUU

MASOMO

KATIKA MATESO YA BWANA

SALA Tuombe haisemwi

Ee Bwana, kumbuka rehema zako, na, kwa ulinzi wako wa milele, uwatakatifuze watumishi wako, ambao Kristo Mwanao aliwawekea fumbo la Pasaka kwa kumwaga damu yake. Anayeishi na kutawala milele na milele.


AU:

Ee Mungu, kwa njia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, uliangamiza mauti, urithi wa dhambi ya kale, iliyokuwa ikitawala vizazi vyote vya binadamu. Utujalie ili, kwa kufananishwa naye, kama tulivyoichukua sura ya mtu wa udongo kutokana na maumbile, kadhalika tuichukue sura ya mtu wa mbinguni, kwa kutakatifuzwa na neema. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SEHEMU YA KWANZA: LITURUJIA YA NENO

SOMO 1: Isa.52:13-53:12

Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo. Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu. Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu. Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea, Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayesimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya, Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki, Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.

WIMBO WA KATIKATI: 

Zab.31:1,5,11-13a,14-16,24.(K)Lk.23:46

1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana

Nisiaibike milele.

Kwa haki yako uniponye,

Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, ee Bwana, Mungu wa kweli.


(K) Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.


2. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,

Naam, hasa kwa jirani zangu;

Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;

Walioniona njiani walinikimbia. (K)


3. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;

Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.

Maana nimesikia masingizio ya wengi;

Hofu ziko pande zote. (K)


4. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)


5. Umwangaze mtumishi wako

Kwa nuru ya uso wako;

Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.

Iweni hodari, mpige moyo konde,

Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)

SOMO 2:

 Ebr4:14-16;5:7-9

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea Yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.


SHANGILIO: Flp.2:8-9

Kristo alijinyenyekeza. Akawa mtii hata mauti, Naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, Akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.


INJILI:

 Yn:18:1-19,42

M. = Msomaji

W. = maneno ya Watu mbalimbali

十 = maneno ya Yesu


M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yalivyoandikwa na Mtakatifu Yohane.


Yesu anakamatwa.

M. Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni; palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu na makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia,

十 Ni nani mnayemtafuta?

M. Wao wakamjibu,

W. Ni Yesu Mnazareti.

M. Yesu akawaambia,

十 Ni mimi.

M. Yuda naye, aliyemsaliti, alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena,

十 Mnamtafuta nani?

M. Wakasema,

W. Yesu Mnazareti.

M. Yesu akajibu,

十 Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi, basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.

M. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro,

十 Rudisha upanga alani mwake; je, kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?


Yesu mbele ya Anasi na Kayafa. Petro anamkana Yesu.

M. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro,

W. Wewe nawe, je, hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu?

M. Naye akasema,

W. Si mimi.

M. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto, Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu,

十 Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; siku zote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.

M. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema,

W. Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?

M. Yesu akamjibu,

十 Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?

M. Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia,

W. Wewe nawe, je, hu mwanafunzi wake mmojawapo?

M. Naye akakana, akasema,

W. Si mimi.

M. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema,

W. Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?

M. Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.


Yesu mbele ya Pilato.

M. Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka. Basi Pilato akawatokea nje, akasema,

W. Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?

M. Wakajibu wakamwambia,

W. Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.

M. Basi Pilato akawaambia,

W. Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!

M. Wayahudi wakamwambia,

W. Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.

M. Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionesha ni mauti gani atakayokufa. Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia,

W. Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?

M. Yesu akamjibu,

十 Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?

M. Pilato akajibu,

W. Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?

M. Yesu akajibu,

十 Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.

M. Basi Pilato akamwambia,

W. Wewe u mfalme basi?

M. Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.

M. Pilato akamwambia,

W. Kweli ni nini?

M. Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia,

W. Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?

M. Basi wakapiga kelele tena, na kusema,

W. Si huyu, bali Baraba.

M. Naye yule Baraba alikuwa mnyang'anyi. Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu. Akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema,

W. Salamu! Mfalme wa Wayahudi!

M. Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia,

W. Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.

M. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia,

W. Tazama, mtu huyu!

M. Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,

W. Msulibishe! Msulibishe!

M. Pilato akawaambia,

W. Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.

M. Wayahudi wakamjibu,

W. Sisi tunayo! sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.

M. Basi Pilato aliposikia neno hilo akazidi kuogopa. Akingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu,

W. Wewe umetoka wapi?

W. Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia,

W. Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha?

W. Yesu akamjibu,

十 Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu, kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.


Yesu anahukumiwa kufa.

M. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua: lakini Wayahudi wakapiga makelele wakasema,

W. Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanye kuwa mfalme humfitini Kaisari.

M. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi,

W. Tazama, Mfalme wenu!

M. Basi wale wakapiga kelele,

W. Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!

M. Pilato akawaambia,

W. Je, nimsulibishe Mfalme wenu?

M. Wakuu wa Makuhani wakamjibu,

W. Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.

M. Basi ndipo walipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.


Yesu anasulibiwa.

M. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa Makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,

W. Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.

M. Pilato akajibu,

W. Niliyoandika nimeyaandika.


Askari wanagawanya mavazi ya Yesu.

M. Nao askari walipomsulibisha Yesu waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana,

W. Tusiipasue, lakini tuipigie kura iwe ya nani.

M. Ili litimie andiko lile linenalo: Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.


Yesu na mamae.

M. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye Mariamu wa Klopa na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,

十 Mama, tazama mwanao.

M. Kisha akamwambia yule mwanafunzi,

十 Tazama, mama yako.

M. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.


Yesu anakufa.

M. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema,

十 Naona kiu.

M. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,

十 Imekwisha.

M. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Yesu anatobolewa ubavu.

M. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli, ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: Watamtazama yeye waliyemchoma.

Yesu anazikwa.

M. Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na udi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.

MAOMBI KWA AJILI YA WATU WOTE

I. Kwa ajili ya Kanisa takatifu

Enyi ndugu wapendwa sana, tuliombee Kanisa takatifu la Mungu, ili Mungu na Bwana wetu apende kulijalia amani, kulikusanya na kulilinda popote duniani. Pia atujalie sisi tumtukuze Mungu Baba Mwenyezi, katika maisha ya amani na usalama.

Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, uliyewafumbulia mataifa yote utukufu wako katika Kristo, uilinde kazi ya huruma yako, ili Kanisa lako, lililoenea popote duniani, liendelee kwa imani thabiti kuliungama jina lako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

II. Kwa ajili ya Papa

Tumwombee pia Baba mtakatifu wetu J., ili Mungu na Bwana wetu, aliyemteua katika daraja ya uaskofu, amlinde, akae mzima na salama kwa ajili ya Kanisa lake takatifu, apate kuliongoza taifa takatifu la Mungu.

Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, ambaye vitu vyote huumbwa kwa uamuzi wako, uyasikilize kwa wema maombi yetu. Umlinde kwa huruma yako huyo Mchungaji mkuu uliyemteua kwa ajili yetu, ili jamii ya wakristo, ambao wewe mwenyewe unawatawala, chini ya huyo Mchungaji mkuu, waongezewe mastahili ya imani yao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

III. Kwa ajili ya kila daraja na cheo cha waamini

Tumwombee pia askofu wetu J., maaskofu wote, mapadri, mashemasi wa Kanisa, na jamii yote ya waamini.

Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, ambaye Roho wako hutakatifuza na kusimamia mwili wote wa Kanisa, utusikilize sisi tunaowaombea watumishi wako, ili wote, kwa msaada wa neema yako, wakutumikie kiaminifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

IV. Kwa ajili ya wakatekumeni

Tuwaombee pia wakatekumeni (wetu), ili Mungu na Bwana wetu azibue masikio ya mioyo yao na afungue mlango wa rehema yake, kusudi, wakiisha kupata maondoleo ya dhambi zao zote kwa njia ya maji ya Ubatizo wa kuzaliwa upya, nao pia wawemo ndani ya Yesu Kristo Bwana wetu.


Sala katika ukimya. 

Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayelisitawisha daima Kanisa lako kwa kulipatia wana wapya Uwaongezee imani na akili wakatekumeni (wetu), ili wakiisha kuzaliwa mara ya pili katika kisima cha Ubatizo, wahesabiwe kati ya jamii ya hao uliowafanya watoto wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

V. Kwa ajili ya umoja wa Wakristo

Tuwaombee pia ndugu wote wanaomwamini Kristo, ili Mungu na Bwana wetu apende kuwakusanya katika Kanisa lake lililo moja na kuwalinda hao, watendao ukweli.

Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayeyakusanya yaliyotawanyika na kuyalinda yaliyokusanywa, ulitazame kwa wema kundi lake Mwanao, ili, wale waliotakaswa kwa Ubatizo mmoja, waunganishwe kwa umoja wa imani na kifungo cha mapendo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

VI. Kwa ajili ya Wayahudi

Tuwaombee pia Wayahudi, ambao Mungu Bwana wetu alinena nao kwanza, ili awajalie wazidi kulipenda jina lake na kuwa waaminifu katika kuishi agano lake.

Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, uliyempa Ibrahimu na uzao wake ahadi zako, usikilize kwa wema maombi ya Kanisa lako, ili taifa hilo ulilojipatia kwanza lijaliwe kuufikia utimilifu wa ukombozi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.


VII. Kwa ajili ya wasiomwamini Kristo

Tuwaombee pia wale wasiomwamini Kristo, ili, wakiangazwa kwa nuru ya Roho Mtakatifu, wapate nao kuingia katika njia ya wokovu.


Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, uwajalie wale wasiomwungama Kristo, na wanaenenda mbele ya uso wako kwa moyo mnyofu, waupate ukweli. Nasi, kwa kuzidi daima katika kupendana na kwa kufanya bidii kulifahamu kikamilifu fumbo la uzima wako, utufanye tuwe mashahidi kamili wa mapendo yako ulimwenguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.


W. Amina.


VIII. Kwa ajili ya wasiomwamini Mungu

Tuwaombee pia wale wasiomwamini Mungu, ili, kwa kuyafuata kwa moyo mnyofu yaliyo mema, wastahili kumfikia Mungu mwenyewe.


Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, umewaumba wanadamu wote, ili wakutafute daima kwa hamu na wakikupata watulie. Tunakuomba utujalie ili, watu wote, licha ya vizuizi vyovyote vya uovu, kwa kuzipokea ishara za wema wako na ushuhuda wa matendo mema ya wale wanaokuamini, wapate kufurahi katika kukuungama wewe uliye peke yako Mungu wa kweli na Baba yetu sisi binadamu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.


W. Amina.


IX. Kwa ajili ya viongozi wa Serikali

Tuwaombee pia viongozi wote wa serikali, ili Mungu na Bwana wetu aelekeze akili na mioyo yao kadiri ya mapenzi yake, kusudi watu wote wapate amani na uhuru wa kweli.


Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, mioyo ya watu na haki za mataifa zimo mikononi mwako. Uwaangalie kwa wema wale wenye madaraka ya kutuongoza sisi, kusudi, kwa majaliwa yako, wadumishe popote duniani usitawi wa mataifa, usalama wa amani na uhuru wa dini. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.


W. Amina.


X. Kwa ajili ya wenye taabu

Enyi ndugu wapendwa sana, tumwombe Mungu Baba mwenyezi, ili atakase ulimwengu na upotovu wowote, aondoe magonjwa, afukuze njaa, ayafungue magereza, azifungue pingu. Wanaosafiri wajaliwe usalama, walio mbali warudi makwao, wagonjwa wapone na wanaokufa waokoke.


Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, ndiwe faraja ya wenye kusikitika, na nguvu ya wanaoteswa. Yafike kwako maombi ya wanaokulilia katika taabu yoyote, ili, kwa rehema yako, wote, kila mmoja katika shida yake, wafurahie kusikilizwa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

SALA BAADA YA KOMUNYO:

Ee Mungu mwenyezi wa milele, umetuhuisha kwa njia ya kifo kitakatifu na ufufuko wa Kristo wako. Tunakuomba, udumishe ndani yetu kazi ya rehema yako, ili, kwa kushiriki fumbo hili takatifu, tupate kuishi katika uchaji siku zote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

SALA JUU YA WATU:

Ee Bwana, tunakuomba, baraka zako nyingi ziwashukie watu wako, ambao wamekumbuka kifo cha Mwanao kwa kutazamia kufufuka kwao; wapate rehema, wajaliwe kitulizo, waongezewe imani takatifu, na wathibitishiwe ukombozi wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies