ALHAMISI, JUMA LA 10 LA MWAKA

MASOMO YA MISA, JUNI 13, 2024

SOMO: 1Fal.18:41-46
Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ile ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanya mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuingia Yezreeli.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.





WIMBO WA KATIKATI: Zab.65:9-12(K)

1. Umeijilia nchi na kuisitawisha.
Umeitajirisha sana;
Mto wa mungu umejaa maji;
Wawaruzuku watu nafaka,
Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.

(K) Ee Mungu, sifa zakulaki katika Sayuni.

2. Matuta yake wayajaza maji;
Wapasawazisha palipoinuka,
Wailainisha nchi kwa manyunyu;
Waibariki mimea yake. (K)

3. Umeuvika mwaka taji ya wema wako;
Mapito yako yadondoza unono.
Huyadondokea malisho ya nyikani,
Na vilima vyajifunga furaha. (K)

SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likaa kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Aleluya!



INJILI: Mt.5:20-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies