ALHAMISI JUMA LA 9 LA MWAKA


MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwabudu Bwana, kwani yeye ni Mungu wetu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifu. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Fahari yake ye Baba
Kristo nuru yetu,
Kwa upendo na huruma
Aja kufanya kivuko
Cha shimo kubwa ajabu,
Shimo kubwa la madhambi
Baina ya wanadamu
Na Mungu Mtakatifu.

Kristo siku ya jana,
Na leo pia Kristo,
Ana hali ile ile,
Habadiliki milele,
Mfano wa Mungu wetu,
Mungu aliyefichika;
Na 'Hekima ya Milele'
Ndilo hasa jina lake.

Neno lake hulishika
Karne hata karne,
Yupo pamoja na sisi
Hadi mwisho wa nyakati;
Mchana Yeye ni wingu,
Usiku mwali wa moto,
Hivyo hututangulia
Katika zakeye njia.

Tunakutukuza Baba
Chanzo halisi cha mwanga,
Kadhalika na Kristo,
Yeye Mwanao mpendwa,
Akaaye ndani yetu
Pamoja na Roho wako:
Ndo Utatu wa milele
Katika Mungu Mmoja.

ANT. I: Kinanda na kinubi, amkeni; nitaiamsha alfajiri.

Zab.57 Kuomba msaada
Zaburi hii hutukuza mateso ya Kristo (Mt. Augustino)

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,*
kwako ninakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako, napata usalama,*
hata hapo dhoruba kali itakapopita.

Namlilia Mungu Mkuu,*
Mungu anijaliaye kila kitu.

Atanisikiliza kutoka mbinguni na kuniokoa;/
atawashinda hao wenye kunidhulumu.*
Mungu atanionesha mapendo na uaminifu wake.

Adui wanizunguka kama simba wala watu;/
meno yao ni kama mikuki na mishale,*
ndimi zao ni kama panga kali.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu,*
utukufu wako uenee duniani kote.

Adui wamenitegea wavu waninase,*
nami nasononeka kwa huzuni.

Wamenichimbia shimo njiani,*
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

Niko imara, Ee Mungu, niko imara;*
nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!/
Amkeni, enyi zeze na kinubi!*
Nitayaamsha mapambazuko!

Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;*
nitakuimbia sifa kati ya watu.

Upendo wako mkuu waenea hata mbinguni,*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Utukuzwe, Ee Mungu, juu ya mbingu;*
utukufu wako uenee duniani kote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kinanda na kinubi, amkeni; nitaiamsha alfajiri.

ANT. II: Bwana asema hivi: Watu wangu watashibishwa mema yangu.

WIMBO: Yer.31:10-14 Furaha ya watu waliokombolewa
Yesu ilimpasa kufa kusudi awaunganishe watoto wa Mungu waliokuwa wametawanyika (Yoh.11:51-52)

Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa,*
litangazeni visiwani mbali; mkaseme,

Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda,*
kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo,*
amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sion,*
wataukimbilia wema wa BWANA,

nafaka, na divai na mafuta,*
na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe;

na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji;*
wala hawatahuzunika tena kabisa.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,*
na vijana na wazee pamoja;

maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,/
nami nitawafariji, na kuwafurahisha*
waache huzuni zao.

Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono,*
na watu wangu watashiba kwa wema wangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana asema hivi: Watu wangu watashibishwa mema yangu.

ANT. III: Bwana ni mkuu, astahili sifa katika mji wa Mungu wetu.

Zab.48 Sion mji wa Mungu
Akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, yaani Yerusalemu (Ufu.21:10)

Mungu ni mkuu na wa kusifika sana,/
katika mji wa Mungu wetu,*
juu ya mlima wake mtakatifu.

Sion, mlima wa Mungu, ni mrefu na mzuri;*
mji wa mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu.

Katika ngome za mji Sion,*
Mungu amejionyesha kuwa mwamba wa usalama.

Wafalme walikusanyika,*
wakaanza kushambulia.

Lakini walipouona tu mji wa Sion, wakashangaa;*
akashikwa na hofu, wakatimua mbio.

Woga uliwashika wakaanza kuhangaika,*
wakawa kama mwanamke anayejifungua.

Uliwarusharusha kama meli katika dhoruba./
Yote tuliyosikia Mungu ametenda,*
sasa sisi wenyewe tumeyaona;

katika mji wa Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
Mungu atauweka mji huo salama milele.

Ee Mungu, twautafakari upendo wako mkuu,*
tukiwa Hekaluni mwako.

Wewe wasifika kila mahali,/
sifa zako zaenea popote duniani.*
Wewe watawala kwa haki;

watu wa Sion wafurahi!/
Wewe watoa hukumu zilizo sawa;*
watu wa mji wa Yuda na washangilie!

Haya, nendeni Sion mkauzunguke,*
nendeni mkahesabu minara yake.

Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake;*
mpate kukisimulia kizazi kijacho, kwamba:

“Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele!*
Atakuwa kiongozi wetu milele"!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana ni mkuu, astahili sifa katika mji wa Mungu wetu.

SOMO: Isa.66:1-2
BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.

KIITIKIZANO
K. Naliita kwa moyo wangu wote: Bwana nisikie. (W. Warudie)
K. Nitazitii amri zako.
W. Bwana nisikie.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Naliita...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Tumtumikie Bwana kwa uchaji, naye atatuopoa mikononi mwa adui zetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Tumtumikie Bwana kwa uchaji, naye atatuopoa mikononi mwa adui zetu.

MAOMBI
Tumshukuru Kristo ambaye ametupatia siku hii mpya, na tumwombe:
W. Bwana, uipokee na kuibariki kazi yetu ya leo.

Ulijitoa mwenyewe kwa Baba badala yetu;
- unganisha majitoleo yetu na yako. (W.)

Wewe ni mpole na mnyenyekevu wa moyo;
- utufundishe kuwapokea wengine kama ulivyofanya. (W.)

Kama jua lichomozavyo kila siku, nuru itokee ndani ya mioyo yetu,
- na ing'ae duniani kwa mapendo. (W.)

Onesha huruma yako kwa wagonjwa,
- ili tumaini lao kwako lipate kuongezeka siku hata siku. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, tunakutolea sala zetu asubuhi, mchana na jioni. Utuondolee mioyoni mwetu giza la dhambi, na utufikishe kwenye mwanga halisi, yaani, Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies