MASOMO YA MISA IJUMAA

MOYO MTAKATIFU WA YESU MWAKA B MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.33:11,19
Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi, yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka fadhili za ajabu za mapendo yake kwetu. Tunakuomba utujalie tustahili kupokea neema tele katika chemchemi hiyo ya karama za mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

Au:
Ee Mungu, kwa huruma yako unapenda kutujalia hazina isiyopimika ya upendo katika Moyo wa Mwanao uliojeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu. Tunakuomba utujalie ili, kwa kumtolea heshima ya ibada yetu, tutimize pia wajibu wa malipizi yatupasayo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Hos.11:1b,3-4,8c-9
Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayari mwao, nikaandika chakula mbele yao. Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya maji.


WIMBO WA KATIKATI: Isa12:2-6(K)3
1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Mungu ni nguvu zangu
na wimbo wangu;
Basi, kwa furaha mtateka maji
katika visima vya wokovu.

(K) Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.

2. Na katika siku hiyo mtasema,
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni, matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)

3. Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)


SOMO 2: Efe.3:8-12,14-21
Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya Kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini. Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele Amina.

SHANGILIO: 1Yoh.4:10
Aleluya, aleluya!
Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu
Aleluya!

INJILI: Yn.19:31-37
Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae Juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku ya Bwana) walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulubiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: watamtazama yeye waliyemchoma.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utazame upendo usio na kifani wa Mwanao mpenzi, ili sadaka tunayokutolea ikupendeze na kuwa kwetu fidia ya dhambi zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Mapendo Makuu ya Kristo.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye aliinuliwa msalabani, akajitoa mwenyewe kwa upendo wa ajabu kwa ajili yetu. Alichomwa ubavu, akamwaga damu na maji, zipate kububujika kutoka humo sakramenti za Kanisa, ili wote wavutwe na huo Moyo wazi wa Mwokozi, na kuchota siku zote kwa furaha neema katika chemchemi hiyo ya wokovu.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Watakatifu na Malaika wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.7:37-38
Bwana asema: Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

Au: Yn.19:34
Askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti hii ya mapendo ituwashie upendo mtakatifu, ambao, kwa kutuvutia daima kwa Mwanao, utufundishe kumtambua yeye katika ndugu zetu. Anayeishi na kutawala milele na milele.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies