MASOMO YA MISA JUMAMOSI JUNI 8

 MOYO SAFI WA MARIA

MASOMO


ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.13:5-6
Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi, ili kuwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, ulimtayarishia Roho Mtakatifu makao stahifu katika Moyo wa Bikira Maria mtakatifu. Uwe radhi kutujalia, kwa maombezi ya Bikira huyohuyo, ili tustahili kuwa hekalu la utukufu wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.61:10-11
Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.

WIMBO WA KATIKATI: 1Sam.2:1-8
1. Moyo wangu wamshangilia Bwana,
pembe yangu imetukuka katika Bwana,
kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu,
kwa kuwa naufurahia wokovu wako;

(K) Ninafurahi sana katika Bwana wa wokovu wangu.

2. Pinde zao mashujaa zimevunjika,
na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,
na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.

3. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
hushusha chini, tena huinua juu.

4. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
humpandisha mhitaji kutoka jaani,
ili awaketishe pamoja na wakuu,
wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;

SHANGILIO: Tim.1:10
Aleluya, aleluya!
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya!

INJILI: Lk.2:41-51
Wazee wake Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kutimiza siku, wakati wa kurudi kwao, Yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walimpomwona walishagaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

Nasadiki husemwa.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uzipokee kwa wema sala na dhabihu za waamini wako zinazotolewa katika kumbukumbu ya Maria mtakatifu, Mama wa Mungu. Tunakuomba zikupendeze wewe, na kutupatia sisi msaada wa huruma yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.2:19
Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kushirikishwa ukombozi wa milele, tunakusihi, ili sisi tunaoadhimisha kumbukumbu ya Mzazi wa Mwanao, tufurahie utimilifu wa neema yako na tujisikie kuongezewa daima baraka za wokovu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies