MASOMO YA MISA JUNE 20

 

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 11 ya Mwaka (Alhamisi, Juni 20, 2024) 

Somo la 1

YbS 48:1–14

Ndipo aliposimama Nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Aliyekufa ulimfufua katika mauti, Kutoka kuzimu, kwa neno la Bwana. Ukawashusha wafalme mpaka shimoni, na watu wateule vitandani mwao. Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi, na nabii ili akufuate nyuma yako. Ulisikia makaripio huko Sinai, na hukumu za kisasi huko Horebu. Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli. Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi. Ndiyo huyo Eliya aliyefunikwa kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote. Hakutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii; kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na mauti yake kazi zake zikawa za ajabu.
Wimbo wa Katikati

Zab 97:1–7

Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.

Moto hutangulia mbele zake,
Nao huwateketeza watesi wake pande zote.
Umeme wake uliangaza ulimwengu,
Nchi ikaona ikatetemeka.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.

Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.

Na waaibishwe wote waabuduo sanamu,
Wajivunao kwa vitu visivyofaa;
Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.

Shangilio

1Sam 3:9

Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
Injili

Mt 6:7-15

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliyembinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Neno la Bwana.........



No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies