Kumbukumbu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua Padre na Mwalimu wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 12 Juni 2024 kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” amesema, Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Juni, linaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua, Padre na Mwalimu wa Kanisa: mhubiri mahiri wa Injili ya Kristo iliyomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Kwa njia ya Neno la Mungu, Kristo Yesu anang’arisha na kupyaisha maisha ya waja wake. Na hii ni njia pia ya kumfahamu Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu utimilifu wa Ufunuo wa Neno la Mungu, tayari kumtangaza na kumshuhudia. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa kwa kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiachilia na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu na kamwe wasitafute njia za mkato katika maisha ya kiroho! Waamini wanaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda makini kwa Kristo na Kanisa lake, kazi inayotekelezwa kwa ufanisi mkubwa na Roho Mtakatifu.
Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Anthoni wa Padua alizaliwa tarehe 15 Agosti 1195 huko Lisbon nchini Ureno. Katika umri wa ujana wake, alijisadaka sana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Anthoni wa Padua alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina katika maisha yake, kiasi cha kuwavuta watu wengi kufanya toba na wongofu wa ndani. Alifariki dunia tarehe 13 Juni 1231, huko Arcella, Padua, Italia, akiwa na umri wa miaka 35 tu, matendo makuu ya Mungu. Papa Gregori wa IX, hapo tarehe 30 Mei 1232, akiwa mjini Spoleto, Italia, akamtangaza kuwa Mtakatifu. Tarehe 16 Januari 1246 Papa Pio XII akamtangaza kuwa Mwalimu wa Kanisa “Doctor Evangelicus” yaani “Mwalimu wa Injili”. Hii ni kutokana na amana na utajiri uliokuwa unabubujika kutoka katika mahubiri yake yaliyokuwa yanapata chimbuko lake katika Injili. Ibada kwa Mtakatifu Anthony wa Padua imeenea sehemu nyingi za dunia.
No comments
Post a Comment