SALA ZA MCHANA

 ALHAMISI JUMA LA 9 LA MWAKA

SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT. I: Ee Bwana, ondoa pazia mbele ya macho yangu, ili nipate kuyaona maajabu ya sheria yako.

Zab.119:17-24 III Furaha katika sheria ya Mungu
Unifadhili mimi mtumishi wako,*
nipate kuishi na kushika agizo lako.

Uyafumbue macho yangu,*
niyaone maajabu ya sheria yako.

Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani;*
usinifiche maagizo yako.

Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa*
ya kutaka kujua daima hukumu zako.

Wewe wawakemea watu wenye kiburi;*
walaaniwe wanaokiuka amri zako.

Uniepushe na matusi na madharau yao,*
maana nimezishika kanuni zako.

Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu,*
mimi mtumishi wako nitajifunza maagizo yako.

Amri zako ni furaha yangu;*
hunipa ushauri mwema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, ondoa pazia mbele ya macho yangu, ili nipate kuyaona maajabu ya sheria yako.

ANT. II: Ee Bwana, uniongoze katika kweli yako.

Zab.25 Kuomba uongozi na ulinzi
Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa (Rom.5:5)

I
Kwako naja, Ee Mungu, kwa moyo wangu wote!*
Nakutumainia wewe, Ee Mungu wangu,

usiniache niaibike;*
adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.

Wote wale wakutegemeao hawataaibika;*
lakini wanaokuasi ovyo wataaibika.

Ee Mungu, unijulishe njia yako;*
naam, unipe mwongozo wako.

Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,/
kwani wewe ni Mungu unayeniokoa;*
ninakutumainia wewe daima.

Ee Mungu, uukumbuke wema wako mkuu;/
uukumbuke na upendo wako mkuu,*
maana vimekuwako tangu milele.

Unisamehe dhambi na makosa ya ujana wangu;/
unikumbuke kadiri ya upendo wako mkuu,*
kwa ajili ya wema wako, Ee Mwenyezi.

Mungu ni mwema na mwadilifu;*
huwapa wakosefu mwongozo.

Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;*
naam, huwafundisha hao njia yake.

Mungu huwalinda kwa upendo mkuu na uaminifu,*
wale wanaozingatia matakwa ya agano lake.

Kwa heshima ya jina lako, Ee Mungu,*
unisamehe uovu wangu, kwani ni mkubwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ee Bwana, uniongoze katika kweli yako.

ANT. III: Unihurumie, Ee Bwana, maana mimi ni maskini, na sina rafiki.

II
Kila mtu anayemcha Mungu,*
atafunzwa naye mwongozo wa kufuata.

Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima;*
na watoto wake watamiliki nchi.

Mungu ni msiri wa watu wanaomcha;*
yeye huwajulisha hao agano lake.

Namtazamia Mungu daima anisaidie;*
yeye peke yake ataniokoa mtegoni.

Uniangalie, Ee Mungu, unionee huruma,*
kwa sababu mimi niko peke yangu, na mnyonge.

Uniondolee mahangaiko yangu;*
uniokoe katika taabu zangu.

Uangalie unyonge wangu na dhiki yangu;*
unisamehe dhambi zangu zote.

Angalia jinsi walivyo wengi adui zangu;*
ona jinsi wanavyonichukia mno.

Uyalinde maisha yangu na kuniokoa;*
nakukimbilia wewe, usikubali niaibike.

Wema na uadilifu vinihifadhi,*
maana ninakutumainia wewe.

Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;*
uwaokoe katika taabu zao zote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu aliwafanya watu wote wafungwa wa ukaidi, ili awadhihirishie wote huruma yake.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Amo.4:13
Angalia, yeye aifanyizaye milima, na kuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; BWANA, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.

K. Vimhimidi Bwana, vitu vyote vilivyoumbwa naye.
W. Vimtukuze na kumsifu milele.

SALA:
Tuombe: Bwana, wewe ambaye saa hii uliwajalia Roho Mtakatifu mitume walipokuwa wanasali, utujalie nasi neema hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Amo.5:8
Mtafuteni yeye afanyaye Kilima na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA, ndilo jina lake.

K. Anastahili utukufu na heshima.
W. Fahari na enzi vi patakatifu pake.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, wewe ni mwanga mtupu, na ndani yako hamna giza. Nuru yako, kwa mng'aro wake wote, ituangaze, ili tuweze kufuata kwa furaha amri zako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Amo.9:6
Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA ndilo jina lake.

K. Mbingu zautangaza utukufu wa Mungu.
W. Anga ladhihirisha kazi ya mikono yake.

SALA:
Tuombe: Bwana, twakuomba utujalie tuweze kuvumilia taabu na magumu kama alivyovumilia Mwanao wa pekee, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies