ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.54:4,6
Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema.
KOLEKTA:
Ee Bwana, uwabariki watumishi wako, na uwaongezee kwa huruma vipaji vya neema yako, ili, wakiwa na ari katika matumaini, imani na mapendo, wadumu daima katika kuzishika kiaminifu amri zako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Yer.23:1-6
Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana. Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana. Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka. Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana. Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.23:1-3,3-4,5,6(K)1
1. Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu;
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
2. Huniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SOMO 2: Ef.2:13-18
Ndugu zangu, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
SHANGILIO: Yn:15.15
Nasadiki husemwa.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.111:4-5
Au:
Ufu.3:20
Bwana asema: Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba kwa wema wako uwe nasi taifa lako. Na sisi uliotulisha mafumbo ya mbinguni, utufanye tuondokane na maisha ya zamani, tuingie katika upya wa uzima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
No comments
Post a Comment