JUMAPILI YA 25 YA MWAKA B
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA:
Bwana asema: Mimi ndimi wokovu wa watu. Katika shida yoyote wataniita, nami nitawasikiliza; nami nitakuwa Bwana wao hata milele.
KOLEKTA:
Ee Mungu, uliyaweka maagizo yote ya sheria takatifu katika upendo kwako na kwa jirani. Utujalie kuzishika amri zako, tupate kustahili kuufikia uzima wa milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Hek.2:12:17-20
Zaidi ya hayo tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu, atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.54:1-4,6(K)4
1. Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe,
Na kwa uwezo wako unifanyie hukumu.
Ee Mungu uyasikie maombi yangu,
Uyasikilize maneno ya kinywa changu.
(K) Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.
2. Kwa maana wageni wamenishambulia,
Wote watishao wanaitafuta nafsi yangu;
Hawakumweka Mungu mbele yao. (K)
3. Tazama, Mungu anayenisaidia;
Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.
Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu,
Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema. (K)
SOMO 2: Yak.3:16-4:3
Hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki, na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani. Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yetu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.
SHANGILIO: Mdo.16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya!
INJILI: Mk.9:30-37
Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njia walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi, na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.
Nasadiki husemwa.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, uwe radhi kuvipokea vipaji vya taifa lako, ili hayo wanayoungama kwa imani na uchaji wayapate kwa njia ya sakramenti za mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO:
Zab.119:4-5
Wewe umetuamuru mausia yako, ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, nizitii amri zako.
Au:
Yn.10:14
Bwana asema: Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi unaotulisha kwa sakramenti zako uwe radhi kutuinua kwa njia ya misaada yako ya siku zote, ili tuyapokee matunda ya ukombozi katika mafumbo na katika mwenendo wetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
No comments
Post a Comment