MTAKATIFU WA LEO : SEPTEMBA 2 | Kumbukumbu ya Mtakatifu. Yusto Askofu na Mtawa

 Tarehe 2 Septemba: Kumbukumbu ya Mtk. Yusto Askofu na Mtawa (390)

Yusto alizaliwa Ufaransa, alikuwa shemasi tu, alipoteuliwa kuwa askofu wa mji wa Lyoni (Ufarasa). Alipokwisha pakwa mafuta matakakatifu ya daraja ya uaskofu, alianza kulisimamia kundi lake kwa bidii. Watu walimsifu na kumpenda kwa wema wake na hekima yake kubwa, na hasa kwa huruma yake kwa maskini. Alikaa Lyoni miaka mingi kwa amani na watu wake wote.

Siku moja palikuwa na mwanamume mmoja aliyekuwa amepoteza akili baada ya kuugua homa kali. Alitokea njiani akapiga upanga kuume na kushoto, akiwaumiza watu wengine. Watu walimzunguka kutaka kumzuia na kumkamata. Akapasua kati akakimbilia kanisani, akaingia humo, kisha akaufunga mlango nyuma yake. Kanisa huwa mahali haramu, wala siyo halali kuingiliwa ovyo kwa sababu ya kumkamata mtu yeyote. Walimfuata, wakakusanyika mbele ya kanisa kwa kelele na vishindo, wakiwa tayari kumulia mbali.

Askofu aliposikia vishindo vya watu, alijingiza kati yao, akajaribu kuwatuliza. Hawakumsikiliza. Kwa hasira, walisema watalichoma moto kanisa, kama askofu asipokubali kumtoa mtu huyo. Askofu akafanya shauri na mzee mmoja, mtu mkubwa wa mji, akapatana naye kwamba atamletea yule mwendawazimu, afungwe chumbani pasipo kudhuiriwa. Basi, askosfu akiamini maneno waliyoagana akaingia kanisani; punde akatoka na yule mkichaa. Lakini maskini, alipofikia kizingitini, hakupata nafasi ya kukingwa na mdhamini wake, akakamatwa mara, akakokotwa njiani, wakamsukuma na kumpiga mpaka wakamwua.

Askofu aliona uchungu sana kwa sababu mtu alikuwa ameuwa baada ya kuamini maneno ya mdhamini wake; kwa saabu hasa imevunjwa sheria iliyokatazwa kumtoa mtu aliyekimbilia kanisani. Ijapokuwa kweli alidanganyika, kwamba  mwenye maagano naye hakuyatimiza maagano, askofu alijipatiliza uuaji huo akakusudia kujitenga na dunia, akae utawani kujitesa hata mwisho wake.

Basi, alipokwisha waza hayo moyoni mwake mbele ya Mungu pasipo kumwambia mtu nia yake, aliondoka kwa siri, akaenda zake hata bandari ya Marsilia (Marseille, Ufarasa), akapanda katika merikebu iliyokuwa tayari kung’oa nanga.Alivuka hata akafika Misri Alishuka akafululiza barani, hata alafika mbugani kwenye nyumba ya watawa. Akaenda kubisha hodi kwenye monasteri. Hakujitaja jina lake wala hakusema kama yeye ni askofu. Akaomba ruhusa ya kutawa kimonaki Alipokelewa, akakaa miaka kadhaa akizoeana na kazi za sala za wenzake.

Hata siku moja akaja mhajiri mmoja kutoka Ulaya. Alipokwisha kuingizwa katika wamonaki waliokaa kitako sebuleni, mara alimtambua Yusto, ndiye askofu wake, kwani naye mwenyewe alikuwa mzaliwa wa Lyoni, mji wake. Alimjongea akamwangukia, akiomba Baraka yake . Abati na wamonaki wengine walihamanika sana, wakamwomba mgeni awape habari. Alipowajulisha wote walimwangukia mtakatifu Yusto wakamwomba radhi kwani hawakumjua kuwa ni askofu. Tangu siku hiyo walimwangukia kwa heshima na kumtukuza; mwenywe hakukubali kupunguza mambo aliyojipasa nayo kwanza. Alifanya kazi, alisali, alifunga pamoja na wamonaki wenzake. Alikaa hivyo maisha yake mpaka akiwa mzee, akafa katika monasteri.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies