Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya 23 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tunamshukuru Kristo Mkombozi, tunamwabudu Kristo Mungu, tunamwomba Kristo Mwenyezi. Kristo Daktari wetu anatuongoza kwa neno lake “Efata” maana yake “funguka.” Jamii ya Kiyahudi ilisumbuliwa na magonjwa kama jamii nyingine. Magonjwa hayo ni macho, ukiziwi, ukoma, kupooza, kifafa na magonjwa ya akili. Leo Neno la Mungu linatuambia kwamba Kristo Yesu ndiye Mganga wa kweli. Manabii walitabiri ujio wake ili kututibu kimwili na kiroho. Nabii Isaya katika Somo la Kwanza (35:4-7a) anawapa moyo Waisraeli utumwani Babeli, “ndipo macho ya vipofu yatakapofumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa…” Unabii huu unatimia Kristo Yesu akimponya bubu kiziwi ili naye ayasimulie matendo makuu ya Mungu. Katika muujiza huu Kristo Yesu hatafuti umaarufu usiokuwa na tija, mvuto wala mashiko, bali anataka kujenga ukimya, ili kuboresha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, tayari kusikiliza sauti yake ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya ukarimu, ili kudumisha ushirika na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.
UFAFANUZI: Mgonjwa huyu anaponywa kwa muujiza. Kristo alimtenga mbali na watu sababu hakutaka umbea, hakutaka habari hiyo ienee kwani watu walimtafsiri vibaya alipoongeza mikate wakataka awe mfalme ili wawe wanakula bure. Kumtenga kuna maana pia ya ubatizo kwani tunatengwa na wasioamini, imani mbovu na tabia zisizofaa, tunakuwa tumechaguliwa, tumeteuliwa na kutengwa na hivi kuwa viumbe wapya tuliomvaa Kristo. Unaikumbuka nguo uliyovishwa ulipobatizwa, ipo wapi? safi? uliagizwa uifikishe safi mbele za Mungu, nyeupe bado? yangu imegeuka rangi. Kama Kristo alivyomtenga bubu kiziwi, tumwombe atutenge na dhambi, atufikishe mbinguni. Ajabu Dk Yesu anamtibu bubu kiziwi kwa kumpaka mate. Kwa wayahudi mate ni pumzi kumbe basi Kristo anamfungua ububu na ukiziwi kwa pumzi yake mwenyewe. nasi tumepokea pumzi hiyo katika Roho Mt. kwa ubatizo ili kutangaza neno lake, ‘sisi sote ni wamisionari, tushike Biblia twende kwa mataifa tukatangaze neno la Mungu’. Kristo anatazama mbinguni, ana hakika Baba anamsikia na kumpeleka Roho wa kweli anayewezesha yote. Halafu Daktari huyu anaamuru kwa mamlaka na uweza ‘ephphatha, funguka!’ nati zinalegea, ulimi unawezeshwa, bubu anasema kiziwi anasikia, alleluia. Tunaposhuhudia makuu haya ya Mungu wafuasi wa leo tufanye nini?
Tumwombe Kristo atufungue ububu na ukiziwi wetu. Nabii Isaya anatuhamasisha kutibiwa na Kristo na kupata furaha, “ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba…”Agizo hili ‘efata!’ limguse kila mmoja wetu. Tufunguke midomo izungumze hekima, itamke mema, imwimbie Bwana, ibariki, isilaani, isiongee matusi, masimango au majungu, midomo ya mwamini iwe ni mlango wa Injili na faraja kwa wenye shida. Efata, funguka! na yafunguke masikio yetu tumsikie Mungu katika neno lake tupate kubadilika, tusikie shida za jirani, tusikie kilio cha wadogo hasa wasio na wa kuwasemea, tusikie uchungu wao tuguswe na mahangaiko yao naye Kristo atatubariki. Efata, funguka! ifunguke milango ya mafanikio na uneemevu katika maisha yako, uvuke vizuizi vyote, Kristo aitie nguvu mikono yako na kukufanikisha katika kujitahidi kwako. Ephphatha, funguka! ifunguke leo jamii yetu inayougua ugonjwa wa ubaguzi na upendeleo. Mt. Yakobo katika somo II (2:1-5) anatuonesha neno hilo. Anatufundisha namna ya kuiishi imani, kwamba tukishabikia baadhi ya watu na kuwadharau wengine tunakuwa bubu viziwi. Neno hili linatuhusu, tunaopendeleana sana.
Mtakatifu Yakobo Mtume anatupa changamoto akisema ‘Je, Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?’ Tusikumbatie umasikini lakini linapokuja suala la huduma, haki, utu na usawa tusibaguane kwa vigezo dhaifu kama hivi, huu ni ububu tena ni ukiziwi, kwanza hakuna mtu mbaya duniani, sote tumevishwa sura na mfano wa Mungu, alleluia. Mwenye mavazi mazuri anahudumiwa kwa wakati, asiye na mavazi ya gharama, T-shirt au shati imepauka sasa ni mwaka 3, khanga ya India akwa akina mama wa kiafrika sasa ina miaka 5, karibu iangaze kila kitu; hana mafuta, sabuni za kunukia, manukato ya kunukia na make up nzuri, nakumbuka kujipaka mafuta ya alizeti au ya shanti enzi hizo.. huyu anapotusogelea ah! hana mvuto, tunamweka kando, tunakuwa bubu viziwi, na hii si Injili… tuonje undugu kwa wote, upendo ni wimbo mzuri, hakuna anayechukia kupendwa, wenzetu wakitupenda, kutujali na kututhamini kwa jinsi tulivyo tunajisikia raha, amani na hivi tunaweza kusali na kuabudu kwa utulivu, mkristo penda, penda, penda ndio Fahari ya ukristo na utu wetu umefumbatwa katika amri hii kuu na kifungo cha ukamilifu na mahusiano kati yetu.
No comments
Post a Comment