MASOMO YA MISA JUMATANO 16 OKT 2024

JUMATANO JUMA 28 LA MWAKA WA 2

Gal.5:18-25

Mkiongozwa na roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri ndiyo haya uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, urushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayo fanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema kama nilivyokwisha kuwaambia ya kwamba watu watendayo mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho na tuenende kwa Roho.


WIMBO WA KATIKATI: 

1. Heri mtu yule asiye kwenda

Katika shauri la wasio haki

Wala hakusimama katika njia ya wakosaji

Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha

Bali sheria ya bwana ndiyo impendezayo

Na sheria yake huitafakari mchana na usiku


(K) Wanaokufuata, Ee Bwana, watakuwa na nuru ya uzima


2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa

Kandokando ya vijito vya maji

Uzaao matunda yake kwa majira yake

Wala jani lake halinyauki

Na kila alitendalo litafanikiwa (K)


3. Sivyo walivyo wasio haki

Hayo ni kama makapi yapeperushwayo na upepo

Kwa kuwa bwana anaijua njia ya wenye haki

Bali njia ya wasio haki itapotea (K)


SHANGILIO:

Aleluya, aleluya!

Maagizo yako yota Ee Bwana ni amini, Yamethibitika milele na milele.

Aleluya!


INJILI:

 Lk.11:42-46

Yesu aliwaambia Mafarisayo: Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wanasheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.



No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies